Nov 07, 2023 02:31 UTC
  • Jumanne, tarehe 7 Novemba, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 22 Rabiuthani 1445 Hijria sawa na 7 Novemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1149 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Musa al-Mubarqa' mtoto wa Imam Muhammad Taqi al-Jawad na ndugu wa Imam al Hadi (as) aliaga dunia katika mji mtakatifu wa Qum, Iran.

Alizaliwa Madina mwaka 214 Hijria na mpaka anafikisha umri wa miaka 6 ambapo baba yake aliuawa shahidi, alikuwa chini ya malezi na usimamizi wa baba yake huyo. Baadaye alijifunza elimu kwa kaka yake, yaani Imam al Hadi (as). Musa al-Mubarqa' kipindi fulani aliishi katika mji wa Kufa katika Iraq ya leo na alipokuwa na umri wa miaka 42 alisafiri na kuelekea katika mji wa Qum, Iran.

Aliishi Qum akijishughulisha na ulinganiaji wa dini ya Uislamu hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. Musa al-Mubarqa' ana daraja ya juu ya kielimu na alikuwa mpokezi wa Hadithi. Aidha alisifika mno kwa taqwa na uchamungu. 

Kaburi la Musa al-Mubarqa'

Katika siku kama ya leo miaka 183 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Taqi Razi, katika mji wa Isfahan nchini Iran.

Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa.

Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku.

Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid". 

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.   

Marie Curie

Katika siku kama ya leo miaka 144 iliyopita, Leo Trotsky mmoja kati ya viongozi wakuu wa mapinduzi nchini Russia alizaliwa.

Alibaidishwa Siberia mara mbili katika zama za utawala wa Tsar kutokana na kujihusisha kwake na harakati za mapinduzi. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Russia, Trotsky alirejea nchini Russia. Hiyo ilikuwa mwaka 1917 na akapatiwa wadhifa wa Kamishna wa Masuala ya Kigeni. Mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Kamishna wa Vita ambapo baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani na Ujerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, alianzisha mapambano dhidi ya wapinzani wa mapinduzi.

Hata hivyo baada ya kuaga dunia Lenin, mwanamapinduzi huyo alishindwa katika vita vyake na Joseph Stalin na mwaka 1925 alibaidishiwa Siberia na baadaye huko Uturuki. Hatimaye aliuawa mwaka 1940 huko Mexico na makachero wa Lenin.   

Leo Trotsky

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Albert Camus mwandishi mashuhuri wa Ufaransa.

Licha ya kuwa familia yake ilikuwa masikini, lakini kutokana na kipaji, bidii pamoja na irada thabiti aliyokuwa nayo, Camus alifanikiwa kupata umashuhuri mkubwa. Mwandishi huyo wa Kifaransa ana vitabu vingi.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Firs Man, The Fall, The Stranger na A Happy Death.

Albert Camus

Na siku kama ya leo miaka 67 iliyopita vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa.

Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la mfereji huo.

Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdulnassir, kuutaifisha mfereji huo.

Vita vya Suez

 

Tags