Jul 02, 2016 21:59 UTC
  • Jumapili, Julai 3, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 27 Ramadhan mwaka 1437 Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Julai 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 877 iliyopita, alizaliwa mjini Andalusia, kusini mwa Uhispania ya leo, Muhyid-Din Abubakr Bin Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn Arabi, msomi mkubwa wa Kiislamu na mtaalamu wa Irfan. Ibn Arabi akiwa na umri wa miaka minane alielekea mjini Seville, moja ya miji maarufu ya Uhispania na kujifunza Qur’an, fiqhi na hadithi. Aidha akiwa kijana, alipata kujifunza elimu ya Irfan na kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Akiwa na miaka 30 Ibn Arabi alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu na kuongeza maarifa ya dini ambapo pia aliandika vitabu mbalimbali. Mwaka 620 alitia kambi mjini Damascus, Syria na kujishughulisha na ufundishaji na kulea wanafunzi sanjari na kuandika vitabu. Kadhalika Ibn Arabi anajulikana kwa mapenzi yake makubwa kwa Ahlu Bayti wa Mtume (saw) hususan Imam Ali bin Abi Twalib (as), ambapo alitaja kwa mapana fadhila nyingi za mtukufu huyo katika vitabu vyake.

Siku kama ya leo miaka 478 iliyopita, alizaliwa katika moja ya vijiji vya mji wa Jabal Amel, nchini Lebanon Hassan Bin Zainud-Din, maarufu kwa jina la ‘Swahibul-Maalim’ msomi wa fiqhi na alimu mkubwa wa karne ya 10 Hijiria. Swahibul-Maalim alikuwa mtoto wa Shahiduth-Thani, alimu mkubwa na maarufu katika uwanja wa elimu ya fiqhi. Alifanya safari mjini Najaf, Iraq kwa madhumuni ya kuendelea na masomo yake ya hawza na baada ya kutabahari katika elimu za fiqhi, usulu fiqhi, mantiki na hisabati alirejea nchini kwake na kujishughulisha na ufundishaji. Miongoni mwa athari za Hassan Bin Zainud-Din ni pamoja na kitabu cha Maalimud-Din. Allamah Swahibul-Maalim alifariki dunia mwaka 1011 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Franz Kafka, mwandishi mashuhuri wa nchini Czech. Baba yake alikuwa mfanyabiashara katili na mwenye akhlaqi mbaya, tabia ambazo zilimfanya Franz Kafka kumuogopa baba yake huyo na hata kumuathiri ukubwani kwake. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alijiunga na chuo kikuu cha Prague na kuchukua shahada ya PHD katika fani ya sheria. Baada ya hapo alijishughulisha na kazi za uwakili na kisha akafanya safari kwa muda mjini Paris, Ufaransa. Franz Kafka alipitia wakati mgumu sana katika maisha yake ambapo alifikia kumchukia kila mtu kiasi cha kumfanya akose marafiki kutokana na dhana mbaya alizokuwanazo kuwahusu watu wengine. Ni baada ya hapo ndipo alipoanza kutalii athari za wataalamu wa fasihi na wanahistoria wa zamani na wengine wa zama zake na taratibu akafikia daraju ya juu katika taaluma ya uandishi. Dhana mbaya zilizotawala maisha ya shakhsia huyo zinaonekana hata katika turathi zake hadi hii leo. Kafka alifariki dunia mwaka 1924 kutokana na maradhi ya kifua kikuu.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita inayosadifiana na 3 Julai 1904, alifariki dunia Theodor Herzl, mwasisi wa harakati ya Kizayuni. Herzl alizaliwa mwaka 1860 mjini Bucharest mji mkuu wa Hungary na kisha kuelekea Austria. Mnamo mwaka 1897 aliasisi Taasisi ya Kimataifa ya Kizayuni kwenye kongamano lililofanyika nchini Uswisi. Herzl alibuni mikakati ya kuasisiwa utawala ghasibu na wa Kizayuni wa Israel kwenye ardhi za Palestina, utawala ambao hadi leo unaendelea kufanya jinai kubwa na kusababisha maafa yasiyo na kifani dhidi ya raia madhlumu wa Palestina.

Siku kama ya leo miaka 3 iliyopita, Muhammad Mursi, rais wa zamani wa Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah el-Sisi wa nchi hiyo. Mursi aliingia madarakani kupitia uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Juni mwaka 2012 na hivyo kuwa rais wa kwanza wa Misri kuingia madarakani kidemokrasia. Mursi hakuweza kutekeleza ahadi zake za kutatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo. Na licha ya kwamba alikuwa na mielekeo ya Kiislamu lakini aliendeleza urafiki na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kama ilivyokuwa katika enzi za dikteta Hosni Mubarak. Kadhalika Muhammad Mursi aliamua kufuata siasa ghalati kuhusu nchi za eneo la Mashariki ya Kati kwa kuwa na uhusiano mzuri na watawala wa Aal-Saudi nchini Saudi Arabia, ambao nao baadaye walimchochea Jenerali Abdel Fattah el-Sisi kumpindua na kumtia mbaroni na viongozi wengine wa harakati ya Ikhwanul Muslimin hadi leo.
Na siiku kama ya leo miaka 28 iliyopita ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran iliyokuwa ikitokea mji wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran kuelekea Dubai, ilishambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama na ugaidi unaotekelezwa na serikali ya Marekani. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao huo pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho cha kigaidi.