Nov 19, 2023 02:31 UTC
  • Jumapili, 19 Novemba, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1445 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 19 Novemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahra (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa. ***

 

Siku kama ya leo, miaka 1437 iliyopita kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur'ani Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye. ***

Vita vya Mu'utah

 

Siku kama ya leo miaka 463 iliyopita, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la 'Abus-Suud', faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu. Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsir Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafruudhaat. ***

Muhammad Mustafa Imadi

 

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, alifariki dunia Franz Schubert mtunzi wa nyimbo maarufu wa nchini Austria. Schubert alizaliwa mwaka 1797 katika familia masikini. Tangu akiwa kijana mdogo alipendelea sana nyimbo huku akiwa na kipawa kikubwa katika uwanja huo na hivyo kuamua kusomea taaluma hiyo. Alianza kubuni nyimbo akiwa kijana na katika umri wake wote aliimba zaidi ya nyimbo 600. Hata hivyo licha ya kuimba nyimbo nyingi hususan mziki wa asili, bado hakuweza kujinasua kutoka kwenye umasikini. Hii ni kwa kuwa nyimbo zake hazikupokelewa kwa wingi na jamii ya wakati wake. Ni baada ya kufariki dunia ndipo nyimbo zake zikapewa umuhimu mkubwa katika jamii. ***

Franz Schubert 

 

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko Allahabad nchini India, Bi Indira Gandhi binti pekee wa Jawaharlal Nehru. Mwaka 1947 baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza na baba yake kuwa Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi alikuwa na nafasi muhimu kando ya baba yake. Mwaka 1964 baada ya kufariki dunia baba yake, Indira Gandhi aliteuliwa katika serikali ya Lal Bahadur Shastri kuwa Waziri wa Habari, Radio na Televisheni. Bi Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia mwaka 1966 hadi 1984 alipouawa. ***

Indira Gandhi

 

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri alifanya safari katika Baitul Muqaddas huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hiyo ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa nchi ya Kiarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Safari hiyo ilifanyika katika fremu ya kujikurubisha Misri kwa utawala haramu wa Israel. Safari ya Anwar Sadat iliwakasirisha mno Waislamu hasa wananchi wa Palestina. Licha ya hali hiyo mwaka 1978 Anwar Sadat alitiliana saini mkataba wa Camp David na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani. Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu zilikata uhusiano na serikali ya Misri zikionyesha kuchukizwa na hatua hiyo ya Sadat ambayo pia ilizusha machafuko na ghasia nchini Misri kwenyewe. Hatimaye mwaka 1981 Khalid Islambuli aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri alimpiga risasi na kumuua Sadat akipinga hatua yake ya kutia saini mkataba muovu wa Camp David. ***

Anwar Sadat

 

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita kundi la kigaidi na kitakfiri la Batalioni ya Abdullah Azzam lililokuwa likiongozwa na gaidi Msaudi Arabia, Majid al Majid ambalo ni miongoni mwa matawi ya kundi la kigaidi la al Qaida, lilishambulia ubalozi wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran mjini Beirut huko Lebanon kwa kutumia magaidi wawili waliojilipua kwa mabomu. Katika mashambulizi hayo mawili ya kigaidi watu 23, akiwemo Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari aliyekuwa Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran nchini Lebanon na mke wa mmoja kati ya wanadiplomasia wa Iran, waliuawa shahidi na watu wengine zaidi ya 160 walijeruhiwa. Walinzi wanne wa ubalozi wa Iran mjini Beirut pia waliuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, Majid al Majid alitiwa nguvuni lakini aliuawa kwa njia ya kutatanisha akiwa katika hospitali ya kijeshi mjini Beirut kabla ya kutoa taarifa yoyote na maiti yake ikakabidhiwa kwa maafisa wa utawala wa Saudi Arabia. ***

Shambulio la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Iran mjini Beirut, Lebanon

 

Tags