Dec 03, 2023 02:30 UTC
  • Jumapili, 03 Disemba, 2023

Leo ni Jumapili 19 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe tatu Disemba, 2023 Miladia

Siku kama ya leo miaka 534 iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa zama hizo alifariki dunia mjini Cairo. Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka 849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Jalaluddin Suyuti kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa. Msomi huyo wa Cairo ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah", "Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa". ***

Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin

 

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafilosofia wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajendra Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950. ***

Dakta Rajendra Prasad

 

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsia, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. ***

Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 3 mwezi Disemba mwaka 1984, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama kulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Wakazi wasio na hatia wa mji wa Bhopal wasiopungua 2500 walipoteza maisha yao na mamia ya wengine pia kujeruhiwa katika janga hilo. ***

 

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.***

Kombora la balestiki

 

Tags