Jul 05, 2016 01:35 UTC
  • Jumanne, Julai 5, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 29 Ramadhani 1437 Hijria sawa na Julai 5, 2016.

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa ajili hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.

Siku kama ya leo miaka 183 iliyopita, alifariki dunia Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo, mnamo mwaka 1826 Miladia, baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo.

Siku kama ya leo miaka 630 iliyopita, alifariki dunia Ibn Furat, faqih, mwanahistoria na mhadhiri wa nchini Misri. Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, kitabu ambacho kinazungumzia historia na matukio ya karne ya sita Hijria.

Na siku kama ya leo miaka 789 iliyopita, alizaliwa Allamah Mutwahhar Hilli, maarufu kwa jina la Jamaluddin, alim, mtaalamu wa hadithi na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu. Awali Jamaluddin alisoma elimu mbalimbali kama vile fiq’hi, usulu fiq’hi na hadithi, kwa baba yake ambapo alifikia daraja za juu katika nyanja hizo. Kuna athari nyingi za vitabu kutoka kwa msomi huyo mkubwa, miongoni mwao ni kitabu kiitwacho “Tadhkiratul-Fuqahaa” Kashful Murad na “Irshaadul-Adh’haan.”