Jan 23, 2024 15:10 UTC
  • Jumanne, tarehe 23 Januari, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 11 Rajab 1445 Hijria sawa na 23 Januari mwaka 2024.

Miaka 1174 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa mjini Baghdad mtaalamu wa fasihi, lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu, Abubakar Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn al Anbari.

Alijifunza elimu ya Hadithi baada ya kukamilisha masomo yake ya lugha na sayansi za Qur'ani tukufu. Ibn al Anbari alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuhifadhi na kushika vitu kichwani mwake. Alikuwa mtu mwema na mchamungu na mbali na kujishughulisha na kufundisha na kulea vizazi vya maulamaa, mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi.

Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya "Adabul Kaatib" na "Dhamaairul Qur'ani." Alifariki dunia mwaka 328 Hijiria akiwa na umri wa miaka 57.

Miaka 874 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa Hadithi Ibn Asakir.

Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata elimu katika vituo vya kielimu vya Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimishqi."   

Miaka 192 iliyopita katika siku kama ya leo Edouard Manet mchoraji mahiri wa Kifaransa alizaliwa. Awali Edouard alikuwa na mapenzi makubwa na ubaharia. Hata hivyo baadaye alianza kujihusisha na uchoraji na kuonyesha kipaji kikubwa katika sanaa hiyo. Kazi zake ziliwavutia wengi. Edouard Manet aliaga dunia 1883.

Edouard Manet

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alizaliwa Sergei Mikhailovich Eisenstein mwananadharia na muongozaji wa filamu wa nchini Russia. 

Aliongoza na kutengeneza filamu yake ya kwanza mwaka 1925 iliyojulikana kwa jina la Strike yaani mgomo. Filamu ya pili ya Sergei Mikhailovich Eisenstein iliyojulikana kwa jina la Battleship Potemkin ilileta mageuzi makubwa katika Sanaa ya filamu na sinema ulimwenguni.

Miongoni mwa athari nyingine za Mikhailovich ni Seed of Freedom, Ten Days that Shook the World na Time in the sun. Mwongozaji filamu huyo aliaga dunia 1948.

Sergei Mikhailovich Eisenstein

Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao.

Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti.

Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa.

Benito Mussolini

Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv.

Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Knesset

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Bahman 1357 Hijria Shamsia, baada ya kupatikana uhakika kuhusiana na uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea Iran akitokea uhamishoni Ufaransa, kuliundwa kamati ya mapokezi ya Imam Khomeini. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 50,000 ikiwa na mjumuisho mkubwa wa wawakilishi kutoka vyama na makundi mbalimbali ya mapinduzi. Jukumu kuu la kamati hiyo lilikuwa ni kumpokea Imam Khomeini, kumlinda, kuweka nidhamu, kulinda usalama na kudhamini mambo ya lazima kwa ajili ya kurejea Imam Khomeini.

Imam Khomeini

 

Tags