Jumapili, Julai 10, 2016
Leo ni Jumapili tarehe tano Mgunguo Mosi Shawwal mwaka 1437 Hijiria, sawa na tarehe 10 Julai mwaka 2016.
Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita, sawa na tarehe 5 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 60 Hijria Muslim bin Aqil binamu yake Imam Hussein (as) aliwasili katika mji wa Kufa moja ya miji ya Iraq, kwa lengo la kuwalingania wenyeji wa mji huo ili kumbai mjukuu huyo wa Mtume (saw). Kabla ya hapo watu wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua kadhaa Imam Hussein AS wakimtaka aende kwenye mji huo na awaongoze kwenye harakati dhidi ya utawala wa kidikteta wa Bani Umayyah. Baada tu ya Muslim Bin Aqil kuwasili katika mji wa Kufa aliwasomea wenyeji wa mji huo barua ya Imam Hussein A.S iliyowakaribisha kujiunga na harakati ya kiongozi huyo. Mwanzoni watu wa mji wa Kufa walikubali ujumbe wa Imam Hussein lakini baadaye wakakengeuka. Mwishowe watu wa Kufa walimsaliti Muslim Bin Aqil na mjumbe huyo wa Imam Hussein akauawa shahidi na askari dhalimu wa utawala wa Bani Umayyah.
Siku kama ya leo miaka 1142 iliyopita, wavuvi wa Norway walivumbua kisiwa cha Iceland kilichopo kaskazini mwa bara la Ulaya na karibu na ncha ya kaskazini. Kisiwa hicho kiliingia katika udhibiti wa Norway mwaka 1261 Miladia na karne moja baadaye, Denmark ikazidhibiti nchi mbili zote yaani, Iceland na Norway. Hatimaye mwaka 1944 Iceland ilifanikiwa kupata uhuru kamili kutoka kwa mkoloni Mdenmark.
Siku kama ya leo miaka 275 iliyopita, ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa miongoni mwa mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, Italia ilijiunga rasmi na Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kipindi hicho Waziri Mkuu wa Italia alikuwa ni Benito Mussolini ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama cha Ufashisti nchini humo. Kuingia Italia katika vita hivyo hakukumsaidia chochote Hitler, licha ya kwamba kulikuwa na taathira kubwa ya ongezeko la uharibifu. Hadi kipindi cha miaka mitatu, Italia ilikuwa imepata hasara kubwa katika sekta tofauti, huku Benito Mussolini akiuzuliwa madarakani na mfalme wa wakati huo wa Italia mwezi Disemba mwaka 1943, kufuatia kudhibitiwa na waitifaki ardhi ya kusini mwa nchi hiyo.
Siku kama ya leo, miaka 76 iliyopita, Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa vita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.
Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa hivyo viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.