Jul 10, 2016 06:31 UTC

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine na kipindi chetu cha leo. Katika kipindi kilichopita tulisema kwamba, dunia ni utangulizi wa harakati na safari ya mja kuelekea kwenye ulimwengu wa milele, usio na mwisho na wa kudumu.

Katika ulimwengu huo mwanadamu atakuwa na aina nyingine ya maisha ya milele. Hata hivyo kunajitokeza swali kwamba, je maisha hayo ya milele yanafanana na haya ya dunia hii ya kupita au yanatofautiana? Na kama yanatofautiana ni zipi tofauti hizo?

Kipindi chetu cha leo kitazungumzia kwa muhtasari tofauti na mshabaha uliopo baina ya maisha ya dunia na maisha ya Akhera. Karibuni…

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, kuna uhusiano na mfungamano mkubwa na wa kina baina ya maisha ya dunia hii na yale ya Akhera. Ulimwengu wa Akhera ni picha kamili na timilifu ya dunia hii na kuna mambo mengi yanayofanana baina na ulimwengu hizo mbili. Vilevile tofauti za ulimwengu hizo mbili ni tofauti za kati ya kiumbe nakisi na pungufu na awamu iliyokamilika na kutimia na kiumbe hicho. Ni mithili ya tofauti za tunda ambalo halijakomaa na changa na aina iliyokamilika na kuwiva ya tunda hilo hilo. Kwa utaratibu huo katika safari yake ya kuelekea kwenye ukamilifu, ulimwengu huu wa maada hatimaye utafikia ukamilifu huko katika ulimwengu wa Akhera. Tunapozungumzia mambo yanayofanana na yanayohitilafiana ya maisha ya dunia na Akhera tunaweza kusema kuwa, kila moja kati ya maisha hayo mawili ni hakika na kweli kwa maana kwamba, katika maisha yote mawili mwanadamu hudiriki na kujua kwamba yupo. Katika maisha ya dunia na ya Akhera kuna ladha na mashaka, furaha na machungu, saada na tabu. Katika maisha yote mawili mwanadamu anaishi akiwa na viungo kamili vya mwili wake. Hata hivyo kuna tofauti za kimsingi pia baina ya maisha ya dunia na ya Akhera. Kwa mfano tu, katika maisha ya dunia hii mwanadamu hupitia awamu mbalimbali za ukamilifu kwa maana kwamba, baada ya kuzaliwa hupitia awamu ya utotoni, ujana, utu uzima na uzee hadi anapofikwa na mauti. Hali ni tofauti katika ulimwengu wa Akhera ambako hakushuhudiwi awamu kama hizo za maisha ya mwanadamu. Katika dunia hii mwanadamu anabanwa na muda maalumu wa umri. Umri wa mwanadamu katika dunia hii una kiwango maalumu ambacho hapana budi kitafikia mwisho wake. Qur’ani tukufu imebainisha suala hilo kwa maneno ya kuvutia katika aya ya 45 ya Suratul Kahaf kwa kuyafananisha maisha ya dunia hii ni mmea ambao hunawiri na kuwa kijani kibichi kwa siku kadhaa kisha huanza kunyauka na kufifia na hatimaye kukauka na kutoweka. Tofauti na maisha ya dunia, maisha ya Akhera ni ya kudumu na milele na aya za Qur’ani tukufu zimeweka wazi uhakika huo.

Tofauti nyingine ya kimsingi baina ya maisha ya dunia na ya Akhera ni kwamba furaha na ladha za dunia zimechanganyika na ghamu, mashaka, tabu na maumivu. Wanadamu wote sambamba na ladha, furaha, utulivu na ukwasi walionao kwa viwango tofauti, huwa na mashaka, ghamu, wasiwasi na misukosuko ya aina mbalimbali. Si sahihi kwamba baadhi ya wanadamu huwa katika neema, furaha na utulivu daima na wengine huwa katika ghamu, mashaka na maumivu siku zote, la hasha. Hata hivyo katika ulimwengu wa Akhera hali huwa tofauti. Ulimwengu huo una sehemu mbili tofauti, Pepo ya Naima na Moto wa Jahannam. Katika Pepo hakuna mashaka, woga, majonzi, masikitiko, tabu na maumivu ya aina yoyote, na katika Jahannam hakupatikani isipokuwa mashaka, maumivu, majuto na tabu za kudumu. Kwa hakika tunapaswa kusema kuwa, mashaka, tabu na maumivu ya Akhera ni shadidi na makali zaidi na zaidi kuliko ya dunia hii. Aya nyingi za Qur’ani tukufu pia zimeweka wazi suala hilo na kufanya ulinganisho baina ya maisha ya dunia na Akhera na kufadhilisha maisha ya Akhera ambako mwanadamu huwa pamoja na Mola Karima.

Tofauti nyingine iliyopo baina ya dunia na Akhera ni kwamba ulimwengu wa Akhera una masharti na sifaa zake makshusi. Kwa mfano katika ulimwengu wa Akhera kuna zama, nyakati na maeneo lakini vinavyotofautiana na zama na maeneo ya kidunia. Kuhusu mwili huu wa kimaada wa mwanadamu inatajwa kwamba, roho ya mwanadamu baada ya kufariki dunia na kumalizika maisha ya dunia hii itakuwa katika mwili mwepesi ambao hauna athari za mwili wa kimaada. Mwili huo mwepesi unaumbika kutokana na amali na matendo ya mja aliyoyafanya katika dunia hii. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, amali na matendo yote ya mwanadamu yana sura mbili, sura ya “kidunia” kwa maana ya kile kinachoonekana hivi sasa, na kwa kuwa ni ya sura ya kidunia basi hapana budi itakufa na kuisha. Mfano wake ni maneno ya mwanadamu ambayo yana kipindi na wakati maalumu, yanaanza wakati fulani na kumalizika katika wakati mwingine. Lakini amali hiyo hiyo ina sura nyingine ya “kiakhera”, ya Siku ya Qiyama na ya batini ambayo haiishi na kutoweka. Sura hii ya amali na matendo ya mwanadamu hubakia milele. Hivyo basi iwapo kwa mfano mwanadamu atamsengenya mwanadamu mwenzake sura ya kidunia ya kitendo hicho ni hii tunayoishuhudia ya maneno yanayotolewa na msengenyaji katika hali maalumu. Na sura na picha ya kiakhera ya kitendo na amali hiyo ni kwamba maneno hayo huwa chakula cha wakazi wa Jahannam. Mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Ali Zainul Abidin (as) anasema: “Jiepusheni na kusengenya kwa sababu kitendo hicho huwa mboga ya mbwa wa Jahannam”.  (Biharul Anwar:78)

Maisha ya dunia na neema zake kadiri zinavyomvutia mwanadamu lakini zinachosha na kukinaisha. Katika maisha ya dunia hii mwanadamu hupatwa na hali ya uchovu, kukosa hamu na kukifu vitu mbalimbali hususan maisha ya aina moja kama kwamba ana kitu anachokitafuta, na anapopata kitu fulani hudhani amepata muradi wake na kukishikilia. Lakini baada ya kupita muda huhisi kwamba amekichoka na kwamba si muradi na matakwa yake halisi. Hivyo huchoka na kuanza kutafuta kitu kingine. Kwa utaratibu huo mwanadamu katika dunia hii daima hutafuta kitu asichokuwa nacho. Ama katika ulimwengu wa Akhera watu wanaoingia peponi hawatapitapi na kupatwa na hali ya uchovu na kukosa hamu, bali huwa wamepata muradi na mahbubu wao waliokuwa wakimtafuta umri mzima na maisha ya kudumu, kamili na ya milele. Qur’ani Tukufu inaashiria suala hilo katika aya ya 108 ya Suratul Kahf inaposema: “Watadumu humo (peponi), hawatataka kuondoka”.

Hivyo baasi watu wa peponi pamoja na kwamba watakaa humo milele lakini kamwe hawashibi na kukinai neema zake.

Tofauti nyingine muhimu baina ya dunia na Akhera ni kwamba maisha ya dunia ni utangulizi wa Akhera na wenzo na chombo cha kutufikisha kwenye saada na ufanisi wa milele. Mkabala wake, maisha ya Akhera ni maisha ya juu kabisa, ya mwisho na asili. Duniani mwanadamu anapaswa kufanyakazi, kupanda mbegu na kutayarisha mazingira mazuri, na huko Akhera anavuna na kuchuma matunda ya kazi, mbegu na miche aliyipanda na kuipalilia hapa duniani. Huko hakuna nafasi wala fursa na kupanda na kuchuma thawabu. Dunia ni sehemu ya kazi na amali na Akhera ni nyumba ya kuchuma na kupewa hesabu za kazi na amali. Katika dunia kuna uwezekano wa mwanadamu kubadili hatima yake kwa kubadili mwelekeo wa safari na harakati na aina ya matendo na amali zake. Ama huko Akhera njia inakuwa tayari imeainishwa na mwanadamu hana uwezo wa kuibadilisha. Hivyo saada na ufanisi katika ulimwengu wa Akhera unafungamana na matendo, mwenendo na amali za mwanadamu mwenyewe hapa duniani.

Uhusiano wa dunia na Akhera si kama uhusiano baina ya vitu vya kidunia. Kwa mfano tu kila mtu mwenye nguvu na uwezo mkubwa zaidi, mzuri zaidi, mwenye furaha na maisha bora zaidi, tajiri zaidi na kadhalika katika dunia hii si lazima kwamba atakuwa miongoni mwa watu wa peponi katika ulimwengu wa Akhera. La sivyo kina Firauni, Qaruna na majabari wengine wangekuwa na saada na hali bora zaidi katika ulimwengu wa Akhera! Vilevile inatupasa kuelewa kwamba watu wengi ambao hapa duniani hawakuwa na nguvu na uwezo, walikuwa maskini, hohehahe na kadhalika lakini kutokana na kutenda amali njema wakawa watu wa juu, wenye nguvu na neema tele katika ulimwengu wa Akhera.

Baadhi ya watu wanadhani kuwa kuna uhusano wa kinyumenyume baina ya neema za dunia na zile za Akhera. Kwa maana kwamba, watu watakaopata saada na ufanisi katika ulimwengu wa Akhera ni wale ambao hawakuneemeka na neema za dunia, na kinyume chake wale walioneemena hapa duniani hawatapata chochote huko katika ulimwengu wa Akhera. Watu wenye fikra hii wameghafilika kwamba, kukumbatia dunia kunakokemewa katika mafundisho ya dini hakuna maana ya kutumia neema za dunia bali kukumbatia na kufia dunia ni kwa mwanadamu kutekwa na ladha, anasa na neema zake, kuzifanya lengo lake kuu na kutumia nguvu yake yote kwa ajili ya kupata neema na ladha hizo japokuwa mwishowe hatafikia matakwa na muradi wake. Na mtu anayetafuta Akhera ni yule ambaye moyo wake haukutekwa na dunia na lengo lake kuu ni maisha ya Akhera japokuwa atafaidika na neema tele za dunia hii. Mfano wake ni Nabii Sulaimaan na Mitume na mawalii wengine wengi wa Mwenyezi Mungu ambao walifaidi neema tele za kidunia na kuzitumia kama merikebu na chombo cha kuwafikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu Karima.

Kwa msingi huo tunaelewa kwamba kufaidika au kutotumia neema za dunia peke yake si alama ya kuwa karibu au mbali ya rehma za Mwenyezi Mungu au sababu ya kupata saada au adhabu na mashaka ya Akhera. Uhakika huu umewekwa wazi katika aya za 15 na 16 za Suratul Fajr.

Kwa muhtasari ni kwamba, kuna uhusiano mkubwa na wa kina baina ya amali na matendo ya mwanadamu na maisha yake huko Akhera kama inavyosema aya ya 30 ya Suratu Aal Imran kwamba: “Na siku ambayo kila nafsi itakakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa na kukuta maovu iliyoyatenda, itapenda lau kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye mwenyewe.. “

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.             

 

Tags