Apr 24, 2024 02:40 UTC
  • Jumatano, Aprili 24, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 24 mwaka 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1472 iliyopita kwa mujibu wa mahesabu ya wanahistoria wengi, iliasisiwa kwa mara ya kwanza taasisi ya kuandika na kutarjumu vitabu duniani hapa nchini Iran.

Uamuzi huo ulichukuliwa na Khosrow Anushirvan, mfalme wa Sasani nchini hapa. Taasisi hiyo ilijengwa sambamba na maktaba na vilikamilishwa kujengwa mwaka huo huo.

Vitabu tofauti vilikusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kutarjumiwa na mfalme huyo alimtuma daktari wake kwenda nchini India kwa ajili ya kukusanya vitabu kwa ajili ya shughuli hiyo. 

Katika siku kama ya leo miaka 1442 ilyopita alizaliwa Abu Tufail A'mir bin Wathilah al Kinani ambaye alikuwa miongoni mwa washairi na mahatibu mashuhuri za zama za awali za Uislamu.

Abu Tufail alikuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na alisuhubiana kwa muda mrefu na Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kushiriki katika vita vya Siffin, Jamal na Nahrawan pamoja na mtukufu huyo.

Abu Tufail alifaidika sana na elimu na maarifa ya mtukufu huyo. Mashari mengi ya A'mir bin Wathilah yanamsifu Mtume Muhammad (saw).   

Siku kama ya leo miaka 1193 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim al Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (as).

Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu katika kizazi cha Mtume walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu Hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu.

Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika eneo la Rey na wapezi wa Ahlul Bait (as) kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara. 

Haram ya Abdul-Adhim Hassani

Katika siku kama ya leo miaka 753 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1271, mtalii Marco Polo wa Venice alianza safari ya kihistoria ya kutembelea bara Asia.

Kabla yake baba na ami yake walitembelea China kupitia njia ya Asia Ndogo na Iran. Baada ya kurejea ndugu wa Polo kutoka Ulaya, Marco Polo akifuatana na baba yake kwa mara nyingine walielekea China na kutembelea ardhi ya nchi hiyo na visiwa vya kusini mshariki mwa Asia.

Baada ya kurejea nchini kwake, Marco Polo aliandika kumbukumbu ya safari iliyoitwa "Maajabu" kuhusiana na hali ya kijiografia ya ardhi za China, Turkemanistan, Mongolia na sehemu za kusini mashariki mwa Asia. Safari ya Marco Polo barani Asia ilichukua karibu miaka 20.   

Marco Polo

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran.

Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku.

Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Tarehe 24 Aprili mwaka 1916 kulianza harakati ya tatu ya raia wa Ireland kwa ajili ya kujipatia uhuru wao kutoka kwa serikali ya Uingereza.

Harakati hiyo ilienda sambamba na kujiri kwa vita vikali vya kidini baina ya Waprotestanti na Wakatoliki. Vita hivyo vilimalizika kwa kufikiwa makubaliano baina ya David Lloyd George, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza na kiongozi wa harakati ya raia wa Ireland waliokuwa wanataka kujitenga hapo mwaka 1922.   

Bendera ya Ireland

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1927 chanjo ya B.C.G iligunduliwa.

Chanjo hiyo iligunduliwa na madaktari wa kifaransa Albert Calmette na Guerin, baada ya kufanya uchunguzi wa miaka mingi. Chanjo ya B.C.G hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB.

Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani kote.   ***

Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Ordibehesht mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita.

Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake mbalimbali za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Lengo la mashambulio hayo lilikuwa ni kutaka kuwakomboa majasusi wake waliotiwa mbaroni wakati wa kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la kijasusi.

Licha ya kuweko mipango makini, kutumiwa vyombo vya kisasa kabisa na mazoezi mengi yaliyofanywa katika eneo linalofanana na hilo ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, lakini mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyotokea Tabas na kupelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kufa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran.