Jun 06, 2024 06:37 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (53)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 53 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 53 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 46.

سَیِّئَةٌ تَسُوءُکَ، خَیْرٌ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ حَسَنَةٍ تُعْجِبُکَ‏

Madhambi na kitu kiovu kinachokusikitisha ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko jambo jema linalokutia majivuno.

Katika silisila ya hikma zake fupi fupi hii ikiwa ni ya 46, Imam Ali AS anatubainishia nukta nyingine muhimu yenye taathira kubwa ya kumlea mwanadamu katika makhusiano yake na Muumba wake. Imam hapa anasema: "Kitendo kibaya na kiovu kinachokuhuzunisha na kukufanya ujute ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kitendo kizuri kinachokupa kiburi na kukutia ghururi."

Moja ya maradhi makubwa ambayo humpofua mtu na kumfanya ashindwe kuona hali halisi ya jambo fulani na kumfanya aone kwamba anamiliki kila kitu na ana uwezo wa kutenda lolote analopenda, ni kiburi, ghururi na majivuno. 

Ghururi ni vile mtu kuona kuwa kila kitu anajifanya kwa nguvu zake mwenyewe na hakuna msaada wowote wa Mwenyezi Mungu. Katika mafundisho ya Imam Ali AS madhambi na jambo ovu ambalo humfanya mtu atubu na kurejea kwa Mola wake ni bora kuliko jambo jema ambalo humpa kiburi na kumfanya amsahau Muumba wake. Wakati mtu anapoteleza na akafanya kosa halafu akajuta na kutubu kikwelikweli, athari za kosa lake huondoka na kusamehewa na Muumba lakini wakati mtu anapotekwa na ghururi na kuona yeye si mtu wa daraja ya kumuomba radhi mtu yeyote, mtu huyu hata akitenda jema katika hali hiyo ya ghururi na majivuno, huwa ni khasara kwake. 

 

Tunasoma katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Sadiq (amani ya Allah iwe juu yake) kwamba amesema: “Mwenyezi Mungu Mtukufu alimteremshia Daud wahyi na kumwambia:

بَشِّرِ الْمُذْنِبینَ وَانْذُرِ الصِّدیقینَ

“Wape bishara njema watenda madhambi na waonye wakweli. Nabii Daud AS alipoona wahyi huo alishangaa kwa sababu alihisi inabidi iwe kinyume chake. Hivyo alitaradhia kwa Muumba wake kwa kusema: Ewe Mola wangu Mlezi, ni vipi jambo kama hilo linawezekana? Mwenyezi Mungu akasema: Wape bishara njema wakosefu na watendao madhambi, wale ambao baada ya kutenda kwao madhambu wanatubu na kurejea Kwangu, hivyo wape bishara njema kwamba nitawatakabalia toba zao na nitawasamehe madhambi yao. Amma kuhusu kuwaonya waja wema na wakweli ni kwamba wanapaswa kuwa na tahadhari muda wote, wasije wakaingia kiburi kwa matendo yao mema wakaghururishwa na ibada na uchaji Mungu wao. 

Katika hadithi nyingine, Imam Sadiq AS amenukuliwa akisema: Watu wawili waliingia msikitini, mmoja alikuwa amemwabudu Mwenyezi Mungu muda mrefu na mwingine alikuwa ni muovu na fasiki. Walipotoka Msikitini, yule aliyekuwa amemwabudu Allah kwa miaka mingi akatoka ni muovu na yule fasiki alitoka ni mcha Mungu. Haya ni kwa sababu fasiki alipoingia Msikitini alitubu toba nasuha, toba ya kweli na akamililia mno Mola wake na akajuta kwa maovu yote aliyoyatenda, wakati yule aliyekuwa amemwabudu Mwenyezi Mungu miaka mingi aliingia Msikitini akiwa na ghururi na majivuno kwa kusahau kabisa kwamba ameweza kumwabudu Allah kwa taufiki Yake Muumba si kwa ujanja na uwezo wake. Ghururi na majivuno yalipukutisha thawabu zote za miaka mingi ya ibada. 

 

Aidha Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema: Siku moja Nabii Musa AS alikuwa amekaa mara Iblis akamjia. Akamwambia: “Nimekuja kukusalimia kwa sababu ya hadhi na cheo chako kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Nabii Musa AS alitumia fursa hiyo kumuuliza: Hebu niambie, ni madhambi gani ambayo mtu akiyatenda, utamtawala? Akasema: “Mtu anapojawa na ghururi na majivuno kwa matendo yake mema na ibada zake nyingi na kudharau madhambi yake na kuyaona ni madogo. 

Wapenzi wasikilizaji! Tunamalizia kipindi chetu cha leo kwa dua ya Imam Sajjad AS alipokuwa anamuomba Allah kwa unyenyekevu mkubwa akisema:

اللَّهُمَّ إِلَیْکَ تَعَمَّدْتُ بِحَاجَتِی، وَ بِکَ أَنْزَلْتُ الْیَوْمَ فَقْرِی وَ فَاقَتِی وَ مَسْکَنَتِی، وَ إِنِّی بِمَغْفِرَتِکَ وَ رَحْمَتِکَ أَوْثَقُ مِنِّی بِعَمَلِی

“Ewe Mola wangu! Nimekuja Kwako nikiwa ni mwenye haja, ni maskini na nisiye na chochote. Ninategemea msamaha na rehema Zako na si kwa kutegemea ibada na matendo yangu. (Imenukuliwa kutoka kwenye Kitabu cha Sahifatus Sajjadiyyah, dua ya 48).