Jul 10, 2024 02:24 UTC
  • Jumatano, Julai 10, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 4 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria sawa na tarehe 10 Julai 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo, miaka 1385 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo.

Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) akiwataka wasimsaidie mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba atamuua mtu yeyote ambaye ataasi amri hiyo.

Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad alifunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa na akawahonga kwa fedha wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala; tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (saw).    ****

 

Siku kama ya leo miaka 1150 iliyopita, wavuvi wa Norway walivumbua kisiwa cha Iceland kilichopo kaskazini mwa bara la Ulaya na karibu na ncha ya kaskazini.

Kisiwa hicho kiliingia katika udhibiti wa Norway mwaka 1261 Miladia na karne moja baadaye, Denmark ikazidhibiti nchi mbili zote yaani, Iceland na Norway. Hatimaye mwaka 1944 Iceland ilifanikiwa kupata uhuru kamili kutoka kwa mkoloni Mdenmark.   

Siku kama ya leo miaka 962 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq.

Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi.

Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua Aya 226 za Qur'ani Tukufu.

Miaka 283 iliyopita katika siku kama hii ya leo ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering.

Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari.

Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani. 

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, Italia ilijiunga rasmi na Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kipindi hicho Waziri Mkuu wa Italia alikuwa ni Benito Mussolini ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama cha Ufashisti nchini humo. Kuingia Italia katika vita hivyo hakukumsaidia chochote Hitler, licha ya kwamba kulikuwa na taathira kubwa ya ongezeko la uharibifu.

Hadi kipindi cha miaka mitatu, Italia ilikuwa imepata hasara kubwa katika sekta tofauti, huku Benito Mussolini akiuzuliwa madarakani na mfalme wa wakati huo wa Italia mwezi Disemba mwaka 1943, kufuatia kudhibitiwa na waitifaki ardhi ya kusini mwa nchi hiyo.   

Siku kama ya leo, miaka 84 iliyopita, Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kwa mujibu wa mkataba wa vita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani. 

Henri Petain

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa hivyo viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.