Jumatatu, 15 Julai, 2024
Leo ni Tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 15 Julai mwaka 2024.
Leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ni siku ya Tasua' yaani tarehe tisa Mfunguo Nne Muharram.
Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong'ona na Mola wake.
Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao.
Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi, lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.
Katika siku kama ya leo miaka 436 kulitokea vita vya Bahari ya Manche (English Channel) kati ya jeshi la majini la Uhispania maarufu kama Jeshi la majini lisiloshindwa na jeshi la majini la Uingereza.
Katika vita hivyo meli kubwa 135 za kivita za Uhispania ziliishambulia Uingereza kwa shabaha ya kulipiza kisasi cha mauaji ya malkia Mary Stuart wa Scotland lakini kutokana na kimbunga kikali meli 85 za Uhispania zilizama majini na kikosi cha jeshi la majini kisichoshindwa cha Uhispania kikapata kipigo kikubwa.
Tangu wakati huo nyota na umashuhuri wa kikosi hicho ukaanza kuzama.
Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, alifariki dunia Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa visa wa karne ya 19 wa Urusi akiwa na umri wa miaka 64.
Chekhov alikuwa tabibu na katika kujitolea alijenga kituo cha tiba ambacho alikitumia katika shughuli hiyo. Baada ya hapo alijiunga na taaluma ya uandishi ambapo alianza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na kuandika makala tofauti wakati huo.
Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na akatokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari".
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, mfalme wa Syria aliyewekwa katika nafasi hiyo na Uingereza alifanikiwa kuwa mfalme wa Iraq baada ya kukimbia kutoka Damascus.
Julai 15 mwaka 1920, baada ya vikosi vya Ufaransa kukaribia mji wa Damascus, Amir Feisal aliyekuwa ametawalishwa na Uingereza huko nchini Syria aliukimbia mji huo. Syria na Lebanon ni miongoni mwa ardhi zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Othmania ambazo mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia ziliwekwa chini ya udhibiti wa Ufaransa.
Tarehe 18 Julai mwaka huo huo, mji wa Damascus ulitekwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya Ufaransa. Amir Feisal ambaye aliongoza Syria kwa miezi mitatu tu akiwa Mfalme, baadaye akatawalishwa na Uingereza kuwa Mfalme wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita yaani tarehe 15 Julai mwaka 1944, jeshi la Marekani lilianza kuishambulia Japan kwa maelfu ya mabomu katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia.
Mashambulio hayo ya mabomu ya Marekani yaliendelea hadi Japan iliposalimu amri. Tukio hilo chungu licha ya kusababisha makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan kuuawa kwa halaiki, lilipelekea pia zaidi ya viwanda elfu tatu vikubwa kwa vidogo kuharibiwa kabisa.
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Nuri Said Pasha Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq aliuawa baada ya kujiri mapinduzi ya umwagaji damu.
AlijIunga na jeshi la utawala wa Othmania akiwa na umri wa miaka 21 na kushiriki katika vita vya utawala wa Othmania na Bulgaria vilivyojiri mwaka 1912. Nuri Said Pasha sambamba na kuwa mwanajeshi, alianzisha harakati za kisiasa na alizingatiwa na Uingereza wakati wa malalamiko ya kisiasa dhidi ya utawala wa Othmania. Hatimaye mwaka 1930 akipata himaya ya Uingereza alichaguliwa kuwa waziri Mkuu wa Iraq.