Jumanne, 12 Novemba, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 10 Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na 12 Novemba 2024.
Katika siku kama ya leo miaka 106 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulikomeshwa nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili.
Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi.
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilimalizika katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani.
Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika.
Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina ya Rafah huko katika Ukanda wa Gaza.
Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 1,000.
Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh, kaka wa Imam Ruhullah Khomeini.
Alisoma masomo ya awali ya kidini kwa maulama na wanazuoni wa mji wa Isfahan na kushiriki masomo ya elimuu ya juu ya kidini kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Baadaye alirejea katika mji wa Khomein na kujishuhulisha na ufundishaji wa fikihi, usuul na masomo mengine.
Ayatullah Pasandideh anayejulikana kama alimu na mujahidi, kipindi fulani alibaidishwa kutokana na upinzani wake kwa utawala wa kifalme wa wakati huo wa Reza Khan na kusimama kwake kidete dhidi ya utawala huo.