Jumapili, 15 Disemba, 2024
Leo ni Jumapili 13 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hiijria sawa na 15 Disemba 2024 Miladia.
Tarehe 13 Jumadithani mwaka 64 Hijria kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi ya wanahistoria, alifariki dunia Fatima bint Huzam al Kulabiyya, maarufu kwa laqabu ya Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Wanahistoria wamehitilafiana juu ya siku aliyozaliwa na baadhi wanasema alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (saw). Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe laqabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba, litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as). Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma wanae wote wanne kwenda kulinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala. Watoto wote wanne wa Hadhrat Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao, Hussein katika medani ya Karbala. Ummul Banin alifariki dunia katika siku kama ya leo mjini Madina na kuzikwa katika makaburi ya Baqi'.

Siku kama ya leo miaka 1016 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo. Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba. Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumi.

Katika siku kama ya leo miaka 192 iliyopita alizaliwa Alexandre Gustave Eiffel mhandisi na msanifu wa mnara mashuhuri wa Eiffel. Umashuhuri wa Alexandre Gustave unatokana zaidi na usanifu na uhandisi wake wa mnara wa Eiffel mjini Paris ulioanza kujengwa tarehe Mosi Julai 1887 chini ya usimamizi wake. Mnara wa Eiffel una urefu wa mita 324 ambapo katika zama zake ulikuwa mnara mrefu zaidi duniani. Alexandre Gustave Eiffel aliaga dunia tarehe 27 Desemba 1923 akiwa na umri wa miaka 91.

Siku kama ya leo miaka 172 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel. Henri ambaye ndiye aliyevumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo, alianza kufanya jitihada za kupata vitu vinavyotoa miali ya X baada ya miali hiyo kugunduliwa na mwanafizikia wa Kijerumani, Wilhelm Conrad Röntgen 8 November 1895. Mwaka 1896 Becquerel aligundua nururishi inayoweza kuzalisha miali ya X. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1908.

Miaka 68 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa mwaka 1901 huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni.

Miaka 49 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 15 Disemba 1975, majeshi ya kikoloni ya Uhispania yalianza kuondoka Sahara Magharibi. Polisario ni moja ya harakati za ukombozi wa Sahara Magharibi iliyowalazimisha Wahispania kukimbia eneo hilo. Harakati hiyo iliundwa mwaka 1973 baada ya wanamapinduzi wa Sahara kuasisi makundi kadhaa ya kupigania ukombozi wa eneo hilo.

Miaka 27 katika siku kama ya leo, iliyopita kanali ya televisheni ya Sahar ya Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Shirika la Redio na Televisheni la Iran ilianza kazi zake kwa kurusha matangazo ya lugha za Kiarabu, Kiazari, Kibosnia, Kituruki, Kifaransa, Kiingereza na Kiurdu. Televisheni za kanali hiyo zinatayarisha na kurusha matangazo mbalimbali yanayolenga familia katika masuala ya kijamii, kisiasa, filamu, sinema za matukio ya kweli, masuala ya kiuchumi na kadhalika. Vilevile televisheni hizo huakisi habari za matukio mbalimbali ya kieneo na kimataifa.
