Jul 28, 2016 06:30 UTC
  • Bani Sadr akiwa pamoja na Rajavi
    Bani Sadr akiwa pamoja na Rajavi

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Shawwal 1437 Hijria sawa na Julai 28, 2016.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita Abul Hassan Bani Sadr, rais aliyeuzuliwa wa Iran alikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Mas'ud Rajavi. Siku 37 kabla yake Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha rais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa Saddam Hussein. Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani. Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevaa nguo za kike.

Bani Sadr na Rajavi

Tarehe 28 Julai miaka 287 iliyopita harakati ya kwanza ya mapambano ya watumwa weusi wa Marekani ilianza huko kaskazini mwa nchi hiyo. Waanzilishi wa harakati hiyo ambao walikuwa watu 44 walimuua kila mzungu waliyekutana naye katika njia yao kutoka Carolina Kusini kuelekea Florida. Lakini walizingirwa na jeshi la Waingereza na kuuawa kabla ya kuingia Florida na kupata uhuru. Baada ya hapo watumwa weusi waliendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kiraia.

Watumwa weusi walikuwa wakitekwa nyara au kununuliwa kutoka Afrika tangu mwanzoni wma karne ya 17 na kupelekwa Marekani kwa ajili ya kuuzwa na kufanyishwa kazi kwa mabwana zao.

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita mkataba wa kihistoria wa Berlin ulisainiwa kati ya wawakilishi wa nchi za Russia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Austria mwishoni mwa mkutano uliofanyika kwa jina hilo. Kongamano la Berlin liliitishwa kufuatia ombi la Bismark, Kansela wa Ujerumani wa wakati huo. Nguvu za kisiasa na kijeshi za Ujerumani ziliimarika zaidi baada ya kusainiwa mkataba huo na hivyo kuiandalia nchi hiyo uwanja wa kuweza kujitanua zaidi. Kusainiwa mkataba wa Berlin mwaka 1878 ilikuwa moja ya sababu zilizoandaa uwanja wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita sawa na tarehe 28 Julai 1976, zilzala kubwa iliukumba mji wa Tank-shan mashariki mwa Uchina. Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 9.7 kwa kipimo cha Rishta iliuwa watu zaidi ya laki sita, kujeruhi mamia ya maelfu na kuwaacha wengine wengi bila ya makazi. Mtetemeko huo wa ardhi ni wa pili kwa ukubwa kuwahi kutokea huko Uchina katika karne ya ishirini na pia ni zilzala kubwa zaidi kutokea nchini humo baada ya ile ya mwaka 1556, iliyouawa watu 830,000.

Na katika siku kama ya leo miaka 325 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.

 

Tags