Feb 16, 2025 02:19 UTC
  • Jumapili, 16 Februari, 2025

Leo ni Jumapili 17 Shaaban 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 16 Februari 2025 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917.  Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. 

Siku kama leo miaka 79 iliyopita, inayosadifiana na 16 Februari 1946 kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu ambazo ni wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya Zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwa na malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto, hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa. 

 

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, sawa na tarehe 16 Februari 1984, Sheikh Raghib Harb, Imam wa Swala ya Ijumaa katika kijiji cha Jibshit cha kusini mwa Lebanon na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon dhidi ya utawala ghasibu wa Israel aliuawa shahidi na vikosi vya utawala huo vamizi. Sheikh Raghib alikuwa mmoja wa wanazuoni wanamapambano amilifu kusini mwa Lebanon kabla ya kuuawa kwake shahidi aliwahi kutiwa mbaroni na makachero wa Wazayuni wavamizi kutokana na mapambano na wito wake wa kuwataka wananchi wasimame na kupambana na Wazayuni. Wakati wa kuzikwa mwili wa shahidi Sheikh Raghib Harb, kulitokea mapigano makali baina ya vijana wa kitongoji cha Jibshit na wanajeshi wa Israel ambayo yalipelekea kuuawa na kujeruhiwa idadi kadhaa ya Waislamu madhulumu wa Lebanon.

Sheikh Raghib Harb

 

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Iran na utawala wa Baath wa Iraq yalianza huko New York Marekani. Katika hali ambayo mazungumzo hayo hayakuwa na natija ya maana na hata kulikuwa na uwezekano wa kuvunjuika kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imethibitisha nia yake njema kwa jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa hususan Katibu Mkuu wake.  

 

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo ilizusha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu kwamba hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon. 

Shahidi Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon