Jumamosi, tarehe 12 Aprili, 2025
Leo ni Jumamosi tarehe 13 Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Aprili 2025.
Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1820, dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona.
Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine.
Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyia majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine.

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1823, alizaliwa Alexandr Ostrovsky mwandishi wa tamthilia wa nchini Russia.
Alihitimu masomo ya sheria katika chuo kikuu ingawa aliamua kujiunga na tasnia ya uandishi wa tamthilia na uigizaji. Karibu kila mwaka Alexandr Ostrovsky alikuwa akifanya uigizaji wa kihistoria au kuandika vichekesho ambapo alikuwa akiakisi hali halisi ya jamii.
Alikuwa na taathira kubwa katika senema ya Russia. Miongoni mwa athari za mwanasanaa huyo ni pamoja na 'Binti wa Barafu', 'Msitu' 'Tufani' na 'Muhanga Mwingine.' Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1886.

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1867, Mutsuhito, mfalme maarufu na mwanamageuzi wa Japan aliingia madarakani nchini humo.
Mfalme huyo aliingia madarakani wakati ambapo Japan ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za udhaifu katika nyuga tofauti. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mutsuhito baada ya mwaka mmoja kuingia madarakani akabuni mapinduzi ya kijamii na kuanzisha mageuzi nchini Japan. Katika uwanja huo alihamisha mji mkuu kutoka Kyoto kwenya Tokyo sambamba na kubadili katiba ya nchi hiyo.
Japokuwa utawala wa Mutsuhito ulifikia tamati mwaka 1912, lakini Japan iliweza kupata maendeleo licha ya kuibuka vita baina yake na China na Russia.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran.
Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu.
Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia.
Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga.
Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.

Na siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita, Muhsin Saba mwalimu na mwandishi wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi katika shule ya Darul Funun alielekea nchini Ufaransa.
Alirejea nchini Iran baada ya kupata shahada ya uzamivu (PhD) na kuanza kufundisha. Dakta Muhsin Saba aliasisi Kundi la Taifa la Utambuzi wa Vitabu. Aidha hakuwa nyuma pia katika kutunga na kuandika vitabu.
