Apr 28, 2025 02:23 UTC
  • Jumatatu, Aprili 28, mwaka 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 29 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 28 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 470 iliyopita, Kongamano la Augsburg lilifanyika katika mji wenye jina hilo huko nchini Ujerumani.

Katika kongamano hilo, viongozi wa Kikatoliki chini ya uongozi wa Papa Paul IV (wa Nne) kwa mara ya kwanza waliunga mkono uhuru wa madhehebu ya Waprotestanti. Katika kongamano hilo pia ulichukuliwa uamuzi wa kurejeshwa mali za Waprotestanti walizokuwa wamenyang'anywa.

Hata hivyo uamuzi huo haukutekelezwa na hivyo kuzusha vita vya miaka kumi kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika nchi mbalimbali za Ulaya. 

Katika siku kama ya leo miaka 241 iliyopita, Ayatullah Agha Muhammad Baqir Wahid Bahbahani fakihi mkubwa wa Kishia aliaga dunia.

Allama Bahbahani ni mmoja wa mafakihi wakubwa zaidi  ambaye licha ya kupita miaka mingi angali anahesabiwa kuwa msomi mbobezi wa taaluma mbalimbali. Allamah Bahbahani aliweka jiwe jipya la msingi la elimu ya Usul na akaihuisha elimu hii muhimu.

Msomi huyu alifanya hima na juhudi kubwa kulinda Ijitihadi na alisimama imara kupambana na mrengo wa Akhbariyuun.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, Benito Mussolini dikteta wa Kifashisti wa Italia aliuawa kwa kunyongwa na wazalendo wa nchi hiyo.

Mussolini alizaliwa Julai 29 mwaka 1883 katika familia masikini huko kaskazini mwa Italia. Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu alianza kufanya kazi ya uandishi katika magazeti. Machi 23 mwaka 1919 Mussolini alistafidi na uasi na hali ya vurugu iliyojitokeza  nchini italia na kuanzisha Chama cha Ufashisti na kuwa kiongozi wa chama hicho.

Ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa 1922 ulimfanya Benito Mussolini kuwa Waziri Mkuu baada ya kumridhisha mfalme.   

Benito Mussolini

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita Marekani ililazimika kuondoka kwa madhila huko Vietnam baada ya kupata kipigo cha kuaibisha.

Majeshi ya Marekani yaliingia Vietnam kwa shabaha eti ya kukabiliana na kasi ya kuenea ukomonisti na kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji waliokuwa maarufu kwa jina la Viet Cong huko Vietnam ya kaskazini. Katika vita hivyo Marekani ilitumia silaha zote zilizopigwa marufuku isipokuwa silaha za nyuklia.

Wapiganaji hao wa mwituni walifanikiwa kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Marekani na tarehe 28 Aprili mwaka 1975 Rais Richard Nixon wa Marekani aliwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuondoka Vietnam. 

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, makundi ya Mujahidina wa Afghanistan hatimaye yalipata ushindi baada ya mapambano ya miaka 13 dhidi ya jeshi la Urusi ya zamani na serikali ya kibaraka ya nchi hiyo.

Baada ya majeshi ya Urusi ya zamani kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 13, hatimaye mwezi Februari mwaka 1989 wanajeshi hao wa Urusi walilazimika kuondoka Afghanistan. Hata hivyo kutokana na makundi hayo ya Kiafghani kutokuwa na mikakati mizuri na pia kutopata misaada kutoka nje, vikosi vya serikali ya Afghanistan viliendelea kubakia madarakani chini ya uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Urusi ya zamani.

Aprili 28 Mujahidina walifanikiwa kuuteka kikamilifu mji wa Kabul na kuiondoa madarakani serikali kibaraka ya Afghanistan.