Israel yaua Wapalestina 30 katika vituo vya misaada vya US, Gaza
(last modified Sun, 01 Jun 2025 07:15:19 GMT )
Jun 01, 2025 07:15 UTC
  • Israel yaua Wapalestina 30 katika vituo vya misaada vya US, Gaza

Vikosi vya utawala haramu wa Israel vimewamiminia risasi Wapalestina waliokuwa wamekusanyika katika vituo vya kusambaza misaada vinavyoendeshwa na kundi linaloungwa mkono na Marekani kusini na katikati mwa Gaza, na kuua shahidi takriban 30 miongoni mwao huko Rafah, huku Mpalestina mwingine akiuawa shahidi karibu na korido ya Netzarim.

Ibrahim Abu Saoud, ambaye alishuhudia shambulizi la Israel dhidi ya watu wanaotafuta misaada karibu na Rafah, amesema wanajeshi wa Israel waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wakielekea kwenye kituo cha usambazaji misaada ya kibinadamu kinachoungwa mkono na utawala huo wa Kizayuni.

"Kulikuwa na watu wengine waliouawa shahidi, wakiwemo wanawake", Abu Saoud, 40, amenukuliwa akisema na shirika la habari la Associated Press. Ameeleza kuwa, "Tulikuwa karibu mita 300 kutoka kwa jeshi la Israel."

Abu Saoud amesema aliona watu wengi wakiwa na majeraha ya risasi, akiwemo kijana mmoja ambaye aliripotiwa kufariki dunia katika eneo la tukio. "Hatukuweza kumsaidia," ameongeza.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa huduma za ambulensi huko Gaza amezungumza na Al Jazeera kuhusu shambulio hilo, na masuala mapana yanayokabili huduma za ambulensi katika eneo la hilo pwani.

Jinai za Wazayuni zisivyowasaza hata watoto Gaza

Amesema vikosi vya Israel vinazuia magari ya kubebea wagonjwa kufika eneo kulikojiri shambulio la bomu mjini Rafah, ili kutoa msaada kwa waliojeruhiwa.

Kwa mujibu wa afisa huyo, wahudumu wa afya wanahatarisha maisha yao ili kuwaokoa waliojeruhiwa kutokana na shambulio la bomu la Israel huko Rafah.

Ameongeza kuwa, vituo vya usambazaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza vimekuwa vituo vya udhalilishaji, na jumuiya ya kimataifa lazima ivizuie.