Waziri Mkuu mpya wa Sudan ala kiapo cha kikatiba
(last modified Sun, 01 Jun 2025 07:13:26 GMT )
Jun 01, 2025 07:13 UTC
  • Waziri Mkuu mpya wa Sudan ala kiapo cha kikatiba

Kamil Idris aliapishwa jana Jumamosi kuwa Waziri Mkuu mpya wa Sudan, mbele ya Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Mpito linalotawala nchini humo.

Kufuatia sherehe za kuapishwa, Burhan na wajumbe wengine wa baraza hilo walikutana na Idris kujadili vipaumbele vya serikali, ikiwa ni pamoja na kuleta utulivu wa uchumi, kulinda maisha ya raia, na kurejesha utulivu katika majimbo ya nchi, imesema taarifa ya baraza hilo.

Uteuzi wa Idris ulirasimishwa Mei 19 kupitia dikrii ya kikatiba iliyotolewa na Burhan, ambaye pia anahudumu kama Kamanda wa Majeshi ya Sudan. Uamuzi huo ulikaribishwa na Umoja wa Mataifa, Kamisheni ya Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD).

Nafasi ya Waziri Mkuu ilikuwa imesalia wazi tangu kujiuzulu kwa Abdalla Hamdok Januari 2022, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Burhan Oktoba 2021.

Hamdok na viongozi wengine wa kiraia walizuiliwa kwa muda kabla ya kurejeshwa chini ya mpango wa kugawana madaraka kwa muda mfupi.

Alijiuzulu wiki kadhaa baadaye, akionya kwamba Sudan ilikuwa "katika hatua ya hatari" huku maandamano makubwa yakizuka kupinga utawala wa kijeshi.

Haya yanajiri huku vita kati ya jeshi la Sudan na waasi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF vilivyoanza mwezi Aprili 2023 na kusababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwafurusha takriban watu milioni 13 kutoka makwao, vikichachamaa.