Jumatano, Septemba 3, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 10 Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na Septemba 3 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1492 iliyopita alifariki dunia babu wa Mtume, Abdul Muttalib katika mji wa Makka.
Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Quraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa nyumba tukufu ya al-Kaaba. Vilevile babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake.
Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as). ***

Tarehe 10 Rabiul Awwal miaka 1473 iliyopita, miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as).
Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu.
Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw) Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe Mtume Muhammad (saw) mbora wa walimwengu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza huko kusini mwa Iran.
Manzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliazimia kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatua ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui.
Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7. ***

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza.
Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa.
Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake, Damascus, ilidhibitiwa na Ufaransa. ***

Miaka 86 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza.
Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo.
Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hitler pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poland bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita.

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza.
Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza.
Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu.
Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.

Na siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, aliaga dunia Dkt. Mahmoud Hesabi mwanafizikia mashuhuri wa Iran anayejulikana kama baba wa fizika ya kisasa ya Iran.
Alizaliwa mwaka 1281 katika mji wa Tehran. Profesa Mahmoud Hesabi alikuwa na bidii kubwa masomoni na daima kuanzia masomo yake ya msingi hadi ya juu alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani. Sambamba na masomo shuleni, Mahmoud Hesabi alikuwa akijihusisha pia na kujifunza na kusoma dafina na hazina ya maarifa ya Kiislamu na Kiirani. Hakutoshoka na taaluma moja tu, bali alifanya hima ya kusoma fani mbalimbali. Alipofikisha umri wa miaka 17, Mahmoud Hesabi alikuwa tayari amefikia daraja za juu za masomo.
Mbali na kuwa mahiri katika taaluma kama za uhandisi wa barabara, majengo, madini, umeme, fizikia na kadhalika, msomi huyu alibobea pia katika lugha za kigeni zilizoenea duniani kama Kiarabu, Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Profesa Mahmoud Hesabi aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 baada ya kuishi maisha yaliyojaa hima na juhudi za kielimu.
