Aug 21, 2016 00:13 UTC
  • Jumapili, Agosti 21, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 18 Dhil-Qaadah mwaka 1437 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Agosti mwaka 2016 Miladia.

Tarehe 21 Agosti inatambuliwa kama siku ya kimataifa ya msikiti. Upasishwaji wa siku hii ulijiri mwaka 1382 Hijiria Shamsia, sawa na tarehe 22 Agosti mwaka 2003 Miladia katika mkutano uliofanyika mjini hapa Tehran na kwa pendekezo la Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la nchini Iran sanjari na kupitishwa na Wizara za Mashauri ya Kigeni za nchi za Kiislamu. Kikao hicho kilifanyika kwa mnasaba wa wiki ya kumbukumbu ya kuchomwa moto msikiti wa Al-Aqsa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel tarehe 21 Agosti mwaka 1969. Aidha katika kikoa hicho nchi za Kiislamu zilitakiwa kutoa himaya kwa misikiti kama mahala patakatifu sanjari na kuienzi.

Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita alizaliwa Augustin-Louis Cauchy, mtaalamu wa hisabati wa Ufaransa.  Cauchy alizaliwa kipindi ambacho nchi hiyo ilikuwa ikishuhudia mapigano ya mapinduzi na ni kwa ajili hiyo ndio maana familia yake ikaelekea kijijini huku Augustin-Louis Cauchy akisoma masomo ya msingi kwa baba yake mzazi.  Akiwa kijana mdogo Cauchy alikuwa na maandalizi ya ajabu katika uwanja wa elimu ya hisabati, ambapo hata kabla ya kutimu umri wa miaka 15 aliweza kutunukiwa zawadi kubwa kutoka kwa mfalme wa nchi hiyo katika uga wa fasihi, huku akihitimu masomo yake akiwa na umri wa miaka 18. Baada ya hapo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya hisabati na kuweza kufikia natija muhimu sana.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, sawa na Agosti 21 mwaka 1969, Masjidul Aqsa kibla cha kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni. Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibiwa vibaya. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv, na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mtuhumiwa huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) ili kukabiliana na hatari zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na matukufu yake.

Masjidul Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu

Siku kama leo miaka 57 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad. Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara, Uturuki. Japokuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo. The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hii katika mkataba huo mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita Wamarekani weusi walifanya maandamano makubwa mjini Alabama kwa ajili ya kutaka kutekelezwa sheria ya usawa nchini humo. Maandamano hayo yalipelekea kuibuka wimbi kubwa la harakati za kutetea haki za kiraia nchini Marekani. Harakati hiyo iliundwa mwaka 1955 kwa lengo la kupatikana usawa kati ya Wamarekani wazungu na wale wenye asili ya Kiafrika nchini Marekani na hatimaye kufikia malengo yake mwaka 1968 kufuatia kupasishwa sheria ya kiraia mwaka huo.