Aug 22, 2016 00:18 UTC
  • Jumatatu, Agosti 22, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Mfunguo Pili Dhil-Qaadah 1437 Hijria mwafaka na tarehe 22 Agosti mwaka 2016.

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada thabiti aliyokuwa nayo ilimuwezesha kuendelea na masomo yake ya fizikia hadi akafika Chuo Kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kilikuwa na uwezo wa kurusha mawimbi ya televisheni hadi umbali wa mita 30 tu na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.

 

Miaka 339 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kukaliwa kwa mabavu La Rochelle.

 

Katika siku kama ya leo miaka 318 iliyopita, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Sharel XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Sharel XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.  Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda.

Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali bin Sina

 

Na siku kama ya leo ya tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Kiirani inatambuliwa kuwa ni siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali bin Sina na inatambuliwa kuwa ni Siku ya Daktari hapa nchini.

Abu Ali Sina mwanafalsafa na tabibu mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani aliyejulikana pia kwa laqabu ya Sheikhul Rais alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Msomi na tatibu huyo mashuhuri wa Kiislamu lijifunza tiba baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.