Aug 27, 2016 00:17 UTC
  • Jumamosi, Agosti 27, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 24 Mfunguo Pili Dhil-Qaadah 1437 Hijria mwafaka na tarehe 27 Agosti mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1237 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Imam Ridha (a.s) aliondoka mjini Madina na kuanza safari yake ya kuelekea Marw kaskazini mashariki mwa Iran ya kale. Imam Ridha alifanya safari hiyo kwa lazima na kwa mashinikizo ya Maamun Khalifa wa Saba wa utawala wa Bani Abbas. Lengo la Maamun kutaka Imam Ridha apelekwe Marw lilikuwa ni kumfanya awe karibu naye na hivyo kudhibiti nyendo zake. Japokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam kuwa mrithi wa kiti, cheo ambacho Imam Ridha alikikubali kwa kulazimishwa, lakini uhakika wa mambo ni kuwa alitaka kuimarisha misingi ya utawala wake. Imam Ridha aliendelea kuutambua utawala wa Maamun kwamba, si halali na alikuwa akifichua uovu na dhulma za utawala huo. Hatimaye Maamun alishindwa kuvumilia shakhsia ya kielimu na kimaanawi ya Imam pamoja na ushawishi wake kwa watu, hivyo akaamua kumpa sumu na kumuua shahidi. ***

Agosti 27 mwaka 1896 yaani miaka 120 iliyopita, kulitokea vita vya muda mfupi zaidi duniani huko visiwani Zanzibar eneo ambalo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jengo la Kihistoria mjini Unguja linalojulikana kwa jina la Beit al-Ajaib lililojengwa na Sultan Barghash bin Said huko Forodhani kisiwani Unguja, lilishambuliwa kwa mizinga ya manowari za Uingereza. Hatua hiyo ilikuja kufuatia ugomvi uliozuka baina ya wana wawili wa Sultani wa Zanzibar. Watoto hao walijulikana kwa majina ya Said Barghash Khalid na Said Hamud bin Muhammad na ugomvi wao ulihusiana na utawala na nani anapaswa kurithi kiti cha ufalme. Vita hivyo vilidumu kwa takribani dakika 38 na kuwa vita vifupi zaidi duniani. ***

Katika siku kama ya leo miaka 1128 Hussein bin Mansour Hallaj Sufi na mshairi wa Kiirani alinyongwa. Alizaliwa kusini mwa Iran na alianza masomo ya dini akiwa kijana mdogo na alipofikisha umri wa miaka 12 alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu. Hallaj mara kadhaa alikamatwa na kutiwa jela huko Baghdad kwa tuhuma za kuendesha harakati dhidi ya utawala wa Bani Abbas. ***

Na miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Moldova iliyoko mashariki mwa Ulaya ilipata uhuru. Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia nchi hiyo ilikaliwa kwa mabavu na tawala, kaumu na nchi mbalimbali zikiwemo, Ukraine, Russia, Romania na utawala wa Othmania. Baada ya mapinduzi ya kikomunisti nchini Russia, Moldova iliungana na Romania. Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Moldova ilikaliwa kwa mabavu na Urusi. Hata hivyo baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, nchi hiyo ikajikomboa na kupata uhur