Ijumaa, Septemba Pili, 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 30 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na tarehe Pili Septemba 2016.
Katika siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi AS mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza huko kusini mwa Iran. Manzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliazimia kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatua ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui. Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7.
Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, yaani tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote. Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya Waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki. Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi Waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani Douglas MacArthur akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan. Mwaka 1951, nchi 49 duniani, zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.