Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (144)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni moja kwa moja kutoka mjini Tehran.
Ni matumaini yetu kuwa hamjambo na mko tayari kusikiliza sehemu ya 144 ya kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambapo swali la kipindi cha leo linasema: Je, Umma wa Kiislamu una majukumu yapi kuhusiana na Maimamu wa Ahlul Beit wa Mtume (saw)? Kuweni pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ili tupate kunufaika na yale tuliyokuandalieni kwa juma hili katika kujibu swali hili muhimu, karibuni.

Ndugu wasikilizaji, tunapokirejea Kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, tunaona kwamba aya zake nyingi zinazungumzia udharura wa kutekelezwa majukumu ya Umma wa Kiislamu kuhusiana na Nabii wa Rehema kwa Walimwengu wote (saw) pamoja na Ahlul Beit wake (as). Jambo lililo wazi ni kuwa majukumu hayo ambayo anapaswa kutimiziwa Mtume Mtukufu (saw) pia yanapaswa kutimiziwa Maimamu watoharifu wa Nyumba yake (as). Tulifafanua na kuzungumzia kwa urefu suala hili katika vipindi vilivyop[ita kuhusiana na majukumu yanayopaswa kutekelezwa a Umma wa Kiislamu kwa Bwana Mtume (saw) au kwa maneno mengine, haki alizonazo kwa Waislamu. Kwa msingi huo tutaashiria hapa baadhi ya majukumu ya pamoja yanayopaswa kutekelezwa na Waislamu kwa Mtukufu Mtume pamoja na Maimamu wa kizazi chake kitoharifu kwa msingi wa masuala yanayoendana na maudhui hii.
Kwa hivyo tunaanza na jukumu la utiifu kwao wote, yaani Mtume na Maimamu ambalo limetajwa katika aya ya 59 ya Surat an-Nisaa inayosema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
Tulizungumzia suala hili la Maimamu wa Ahlul Beit Katika Qur’ani kwa kutumia hoja na dalili za kuamianika za kiakili na hadithi ambapo tuliona kwamba maana na makusudio halisi ya neno ‘Ulil Amr’ katika aya hii ni Maimamu kumi na wawili wa Nyumba ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Hivyo tutatosheka hapa kwa kutaja baadhi tu ya nukta zinazoashiria utiifu huu kwao, endeleeni kuwa nasi.

Nukta ya kwanza ni kuwa amri ya kutiiwa Maimamu wa Ahlul Beit (as) ni ya moja kwa moja na isiyobanwa wala kushurutishwa na jambo lolote lile kama inavyoonekana wazi katika matini ya aya tuliyotangulia kuisoma katika kipindi hiki, jambo ambalo limekiriwa pia na wafasiri wengi wa Ahlu Sunna akiwemo Fakhr ar-Razi katika tafsiri yake ya al-Kabir. Hii ina maana kwamba kuwatii watukufu hawa ni sawa na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw), na wala sio mfano wala katika kiwango cha kuwatii wazazi wawili, ambapo utiifu kwao umeshurutishwa na kufungamanishwa na kutomuasi kwao Mwenyezi Mungu. Twaa ya aina hii kwa Maimamu watukufu haifanani kabisa na utiifu tunaowaonyesha watu wengine wa kawaida wasiokuwa maasumu kwa sababu hakuna dhamana yoyote ya kuthibitisha kwamba baadhi ya amri wanazozitoa huwa hazina makosa katika kuainisha makusudio ya jambo fulani seuze ziwe zimetokana na matamanio au mapendeleo yao binafsi.
Kutengewa Maimamu utiifu huu maalumu ambao ni wa moja kwa moja na ambao haushurutishwi na jambo lolote lile kunatokana na umaasumu wao mutlaki ambao unafanana na ule wa Bwana wao Muhammad al-Mustafa (saw). Na hili ni jambo ambalo linathibitishwa wazi na aya hii ya twaa yenyewe pamoja na aya nyinginezo kama vile aya ya Tat’hir na aya ya as-Swadiqeen, au wasadikishaji.
Jambo hili pia linathibitishwa na hadithi nyingi ambazo zimepokelewa na madhehebu zote mbili za Kiislamu za Shia na Suni kama hadithi ya Thaqalain yenyewe. Mfano wa hadithi hizi ni ile iliyonukuliwa na Ibn Hajar katika kitabu chake cha as-Swawaiq akinukuu hadithi ya at-Tabarani kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: ‘Wala msivitangulie viwili hivi - yaani Qur’ani Tukufu na al-Itra (Ahlul Beit) - msije mkaangamia, wala msivipuuze msije mkaangamia wala msiwafundishe, yaani al-Itra (Ahlul Beit), kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kukulikoni nyinyi.’
Hadithi nyingine inayozungumzia umutlaki wa kutiiwa Ahlul Beit bila ya masharti yoyote yale ni hadithi ya Safina ya Uongofu. Kwa mfano imepokelewa katika kitabu cha Mustadrakul Hakim hadithi iliyonukuliwa na Muslim na Buhkari katika vitau vyao vya hadithi hadithi hii kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) ambayo inasema: ‘Hakika mfano wa Ahlul Beit wangu miongoni mwenu ni mfano wa safina ya Nuh, mtu anayeipanda huongoka na anayekataa kuipanda hughiriki.’
Kwa hivyo kukiuka na kutotii amri zao ni sawa na kughiriki kwenye kiza la upotovu wa Ibilisi na hili ndilo jambo ambalo linasisitizwa na kutiliwa mkazo moja kwa moja na hadithi nyingine ya Mtume ambayo imenukuliwa na Hakim katika kitabu chake cha Mustadrak na vitavu vingine mashuhuri vya Ahlu Suna kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) ambayo inasema: ‘Nyota ni amani kwa walimwengu dhidi ya kughiriki na Ahlu Beit wangu ni amani kwa Umma wangu dhidi ya hitilafu. Hivyo Basi iwapo kabila lolote katika Warabu litawapinga, litahitilafiana na kuwa katika kundi la shetani.’

Wapenzi wasikilizaji, nukta ya pili inayohusiana na wajibu wa kutiiwa amri ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) bila ya sharti lolote ni kuwa twaa na utiifu huu hauhusiani na amri zao za maneno tu bali unajumuisha pia vitendo na mienendo yao yote na kuwafuata katika hali zote, kama anavyoashiria hilo sahaba mkubwa na wa karibu zaidi wa Mtume Mtukufu, katika hadithi ya mji wa elimu ya Mtume na hadithi nyinginezo, al-Imam Amir al-Mu’mineen (as), kama anavyonukuliwa katika kitabu mashuhuri cha Nahjul Balagha. Amesema: ‘Tazamani Ahlu Beit wa Mtume wenu na elekeeni wanakoelekea wao na fuateni athari (nyayo) zao. Hii ni kwa sababu hawatakuondoeni kwenye uongofu wala kukurejesheni kwenye maovu. Wanapoketi basi na nyinyi ketini na amkeni wanapoamka. Msiwatangulieni mkaja mkapotea wala msiachwe nyuma nao mkaja kuhiliki.’ Amir al-Mu’mineen pia anasema: ‘Kizazi cha Mtume (saw) hakifananishwi na yeyote yule kwenye Umma huu. Wao ndio msingi wa dini na nguzo ya yakini….haki ya Wilaya (uongozi wa Umma wa Kiislamu) ni yao pekee yao, na miongoni mwao kuna wasia na urithi.’ Kwa maana ya urithi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika uongozi wa Umma wa Kiislamu.
Kwa msingi wa yale tuliyojifunza katika kipidi cha juma hili, wajibu wa kwanza wa Waislammu kwa Maimamu wa Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw) ni wajibu wa utiifu mutlaki kwao na kufuata nyayo na nyenendo zao kikamilifu katika kila jambo ambapo kwa kufanya hivyo tutakuwa tumejidhaminia mafanikio na ushindi maishani. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kutupa taufiki ya kuwafuata kikamilifu watukufu hawa katika kila jambo tunalolifanya maishani kwa ajili ya kumridhisha Yeye tu.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunakamilisha kipindi chetu cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoyakutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.