Nov 11, 2016 03:00 UTC
  • Ijumaa, 11 Novemba, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Safar 1438 Hijria sawa na 11 Novemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.

Yasser Arafat

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani. Katika karne ya 16 Miladia, wakoloni wa Kireno walianzisha kituo muhimu cha biashara katika pwani ya Angola na kuanza ukoloni wao wa pande zote katika ardhi hiyo.

Ramani ya Angola

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.

Dakta Jonas Salk

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.

Mkatawa wa kukomesha Vita vya kwanza vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".

Nima Yushij

Na tarehe 21 Aban miaka 102 iliyopita wanazuoni wakubwa wa Kishia nchini Iraq walitoa fatwa ya wajibu wa kupambana na uvamizi wa Uingereza ncini humo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Wakati huo ardhi ya sasa ya Iraq ilikuwa chini ya udhibiti wa utawala wa Othmaniya ambao askari wake hawakuwa na uwezo wa kukabiliana na wakoloni wa Kiingereza. Japokuwa walikuwa wakibaguliwa na kudhulumiwa na utawala wa Othmaniya, lakini Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Iraq walikusanyika pamoja na kuanza kupambana na wavamizi wa Kiingereza kwa ajili ya kuilinda nchi yao kutokana na fatwa ya wanazuoni na viongozi wao wa kidini. Kuwepo kwa baadhi ya wanazuoni na maulamaa katika safu za mapambano dhidi ya wakoloni kulizidisha moyo na mori wa mapambano kati ya wananchi. Hata hivyo askari wa utawala wa Othmaniya ambao walikuwa wakiwatambua Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa ni tishio kubwa zaidi kwa utawala wao walianzisha njama za kuwadhoofisha na hatimaye Uingereza iliweza kuidhibiti Iraq. Pamoja na hayo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Iraq kwa mara nyingine tena walifanikiwa kuwafukuza wakoloni wa Kiingereza nchini humo kwa msaada na chini ya uongozi wa wanauozi wa dini.    

Vita vya Kwanza vya Dunia

 

Tags