Dec 04, 2016 04:45 UTC
  • Jumapili, 4 Disemba,  2016

Leo ni Jumapili, tarehe 4 Rabiul Awwal mwaka 1438 Hijria Qamaria inayosadifiana na 4 Disemba 2016

Katika siku kama ya leo miaka 337  iliyopita yaani mwaka 1679 Miladia Thomas Hobbes mwanafalsafa mashuhuri wa Kiingereza aliaga dunia. Alizaliwa tarehe tano Aprili mwaka 1588 Miladia. Alimaliza masomo yake katika Chuo Kikuu Oxford nchini Uingereza na alifanya utafiti mkubwa kuhusiana na falsafa. 

Aliathiriwa sana na fikra za mwanafalsafa Mtaliano Niccolò Machiavelli na alijifunza mengi kutokana na yaliyokuwa yakijiri duniani. Aliamini kuwa mfalme alipaswa kuwa na utawala usio na mipaka na kwamba watu hawapaswi kulalamikia mtawala hata kama malalamiko yao ni sahihi na kwamba walalamikaji walipaswa kukandamizwa. Mwanafalsafa huyo wa Kiingereza alifariki dunia  tarehe 4 Desemba mwaka 1679 akiwa na umri wa miaka 91. ***

Siku kama ya leo miaka 252 iliyopita alifariki dunia huko Karbala, Iraq faqihi, mpokezi wa hadithi, mhakiki na mwandishi maarufu wa Kiislamu katika karne ya 12 Hijria Sheikh Yusuf Bahrani. Alijifunza elimu ya msingi kwa baba yake na baadaye alielekea Bahrain na Makka kwa ajili ya kupata elimu ya juu. Baadaye alielekea katika mji wa Fasa kusini mwa Iran ambako alianza kufundisha na kuandika vitabu. Wakati huo alianza kuandika kitabu chake kikubwa zaidi cha fiqhi kinachoitwa "al Hadaiqun Nadhirah". Mwanzuoni huyo ameandika vitabu 32 katika taaluma mbalimbali vikiwa ni pamoja na "Anisul Musafir" na "Jalisul Khawatwir.''

Miaka 181 iliyopita katika siku kama ya leo, Mirza Abul-Qassim Qaim Maqam Farahani mmoja wa waandishi na wanasiasa wa Iran aliauawa katika kipindi cha utawala wa Qajar. Aliteuliwa kuwa kaimu wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Qajar na baadaye kuchaguliwa kuwa Kansela wa Muhammad Shah. Qaim Maqam Farahani alifanya huduma na kuchukua hatua nyingi za marekebisho nchini Iran. Hata hivyo wasiomtakia mema wa ndani ya Iran na wakoloni wa nje ambao hawakufarahishwa na mambo aliyokuwa akiyafanya yaliyokuwa yakipingana na maslahi yao haramu waliandaa uwanja wa kumuua mwanasiasa huyo.

Miaka 117 iliyopita, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu. Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright.

Na Miaka 64 iliyopita, yaani mwaka 1952 katika siku kama ya leo, mkutano wa pande tatu wa Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini. Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin. Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti. Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961.

 

Tags