Jumatano 07 Disemba, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 7 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 7, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1096 iliyopita Ali bin Muhammad Tanukhi alimu, mwandishi na malenga mashuhuri wa karne ya nne Hijria aliaga dunia huko katika mji wa Basra, kusini mwa Iraq akiwa na umri wa miaka 64. Ali Tanukhi alizaliwa huko Antakia mashariki mwa Uturuki ya leo na akiwa kijana alielekea Baghdad na kuasisi makazi yake. Ali bin Muhammad Tanukhi alikuwa mahiri katika lugha na fasihi ya Kiarabu na kuwa miongoni mwa malenga mashuhuri wa zama hizo. Mbali na kutunga diwani yake ya mashairi ambayo imebaki kama kumbukumbu hadi hii leo, Tanukhi aliandika pia vitabu mbalimbali kimojawapo kikiwa ni kile alichokipa jina la al Arudh.
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929.
Miaka 75 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl Harbor. Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilikuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ilitangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia.
Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Abdul Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni.