Dec 12, 2016 05:06 UTC
  • Jumatatu, 12 Disemba, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 12, 2016.

Siku kama ya leo miaka 1490 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume.

Msikiti wa Quba

Katika siku kama ya leo tarehe 12 Rabiul Awwal miaka 1197 iliyopita, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alifanya safari

katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ndiye mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha al Musnad.

Ahmad bin Hanbal

Siku kama ya leo miaka 277 iliyopita Sayyid Ali Tabatabai alimu mkubwa wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Kadhimain moja ya miji muhimu ya Iraq. Sayyid Ali Tabatabai alisoma masomo ya awali kwa baba yake aliyekuwa alimu na msomi mtajika na baada ya kubobea katika elimu akawa mwalimu na kufanikiwa kulea wanafunzi wengi waliokuja kuwa wasomi wakubwa baadaye. Alimu huyo baadaye alianza kufanya utafiti na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Riyadh al-Masail, sherhe ya kitabu cha Mafatiih cha Feiz Kashani na sherhe ya Mukhtaswarun Nafi'i.

آیت الله سید علی بن محمد طباطبایی

Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya. Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Markoni ambaye baadaye alivumbua pia redio. Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani.

Mwanafizikia wa Italia, Markoni

Tarehe 12 Disemba 1963, yaani miaka 53 iliyopita, Kenya ilifanikiwa kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi na mkoloni huyo. Sambamba na kukoloniwa rasmi nchini hiyo, Jomo Kenyata aliongoza harakati za kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950. Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchi humo. Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.

Bendera ya Kenya

Katika siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, Majlisi ya Waasisi nchini Iran ambayo iliundwa kwa ajili ya kuhamisha mfumo wa kisultani kutoka silsila ya Qajar hadi utawala wa kifalme wa Pahlavi, ilitekeleza kazi yake kwa kufanya mabadiliko ya kimsingi katika Katiba ya Iran. Kwa msingi huo utawala wa miaka 153 wa wafalme wa Kiqajari nchini Iran ulifikia kikomo na badala yake ukaanza utawala wa miaka 53 wa Pahlavi hapa nchini.

Majlisi ya Waasisi nchini Iran