Jumanne, Disemba 13, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 13 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 13, 2016.
Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Sheikh Mahmood Shaltoot Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar na Mufti Mkuu wa zamani wa Misri aliaga dunia. Mwanazuoni huyu mkubwa wa Misri alizaliwa mwaka 1892 nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 14 alianza masomo ya shule ya upili katika Chuo cha Kidini cha Alexandria kilichokuwa tawi la Al Azhar. Alipata chetu cha chuo kikuu mwaka 1918 na kuanza kufunza katika chuo hicho hicho na kisha hatimaya akahamia chuo kikuu cha al Azhar mwaka 1927. Alizidi kupanda cheo kieleimu na kuteuliwa kuwa mwanachama wa baraza la Fatwa chuoni hapo. Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar ambapo alitoa huduma kubwa. Kati ya hatua muhimu alizochukua Sheikh Shaltut katika kipindi cha uongozi wake ni jitihada za kuimarisha umoja na mshikamano kati ya madhehebu za Kiislamu. Baada ya kuandikiana barua kadhaa na Ayatulahil Udhma Borujerdi aliyekuwa marjaa na kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Sheikh Shaltut alitambua rasmi madhehebu ya Shia Ithnaashari. Aliamrisha madhehebu ya Shia yafunzwe katika Chuo Kikuu cha Al Azhar sawa na madhehebu zingie za Kiislamu. Aidha alitoa fatwa mashuhuri na kusema kuwa, inajuzu kwa Mwislamu yeyote kufuata madhehebu ya Shia Jaafariya. Sheikh Shaltut aliaga dunia mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 72.
Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq alitiwa mbaroni akiwa katika maficho yake karibu na Tikrit huko kaskazini mwa Baghdad. Saddam alijificha katika eneo hilo baada ya Iraq kuvamiwa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwezi Machi 2003. Kutiwa nguvuni dikteta huyo wa Iraq aliyemwaga damu za raia wengi wa nchi hiyo kuliwafurahisha sana Wairaki na nchi kama vile Iran na Kuwait ambazo zimepatwa na maafa makubwa kutokana na udhalimu za Saddam Hussein dhidi ya nchi hizo. Katika upande mwingine, pamoja na kuwa walimwengu walikuwa wakisubiri kwa hamu kusikia jinai zilizotendwa na dikteta huyo wa zamani wa Iraq wakati wa utawala wake, Marekani ilimweka dikteta huyo chini ya uangalizi wake baada ya kumtia nguvuni lengo likiwa ni kuzuia kufichuliwa ushirikiano wa karibu uliokuwapo kati ya dikteta huyo na serikali za Magharibi khususan Ikulu ya Rais wa Marekani, White House.
Na siku kama ya leo miaka 1148 alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu. Jorjani alifunzwa masomo hayo ya kidini na Qadhi Mkuu wa mji wa Rei ulioko karibu na Tehran ya leo. Qadhi Jorjani ameandika vitabu vingi kma "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhib al Tarikh". Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa huko Jorjan au Gorgan ya leo kaskazini mashariki mwa Iran.