Jan 26, 2017 08:09 UTC
  • Sayansi na Teknolojia 4

Karibuni katika mjumuiko huu wa vipindi ambavyo huangazia maendeleo mapya katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba duniani na hasa nchini Iran.

Wanasayansi Wairani wamefanikiwa kuunda chombo cha kupima uwezo wa kunusa

Katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, kila siku kunaibuka mahitaji na ulazima wa uundwaji na uvumbuzi wa mbinu na mashine mbali mbali za kuboresha maisha ya kila siku ya mwanadamu. Ni kwa msingi huo ndio wanasayansi Wairani hivi karibuni wakaunda chombo maalumu cha kubaini uwezo wa mwanadamu kunusa. Hii ni mara ya kwanza kwa chombo cha kiwango hicho kutumika kubaini uwezo wa mwanadamu kunusa nchini Iran.

Chombo hicho ambacho kwa Kiingereza kinajulikana kama Smell Identification Test (SIT) hutumika kufanya majaribio katika pua na hivyo hubaini iwapo kuna tatizo au la katika uwezo wa mwanadamu kunusa.

Chombo cha SIT kilichotengenezwa na Wanasayansi Wairani ambacho kimepewa jina la Iran-SIT kimeundwa kwa ajili hasa ya kutibu matatizo ya uwezo wa kunusa yanayotokana na uchafuzi wa hali ya hewa.

Hali kadhalika chombo hicho kinaweza kutumika kutabiri magonjwa ya mfumo mkuu wa neva katika ubongo kama vile Alzheimer na pia kuchunguza matatizo ya kukua watoto kama vile Autism. Mbali na hayo, chombo hicho pia kinaweza kutumika katika zahanati na kiliniki na pia katika vituo vya utafiti wa kitiba.  Aidha chombo cha Iran-SIT kinaweza kutimika katika mashirika ambayo yanahitaji watu wenye uwezo wa kunusa.

Tunaendelea na makala yetu hii ya kuangazia mafanikio ya wanasayansi na watafiti Wairani katika Kituo cha Utafiti cha Royan ambao wamefanikiwa kugundua mada za proteini ambazo huchangia kuwepo utasa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika, kuwepo kiwango cha juu sana cha proteini ni moja ya sababu za  utasa miongoni mwa wanawake wanaougua ugonjwa wa mayai unaojulikana kwa Kiingereza kama Polycystic ovarian syndrome, au PCOS ambao hupunguza uwezo wa mfuko wa uzazi kuhimili kijusi.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kimataifa  la Journal of Research in Medical Sciences (IJRMS). Proteini hiyo ambayo wanasayansi Wairani walifanikiwa kuigundua huwa inachangia utasa na inajulikana kama Apolipoprotein A1.

Kwa mujibu wa watafiti wa Kituo cha Utafiti cha Royan, proteini ya Apolipoprotein A1 huonekana kwa kiwango kikubwa sana katika mayai ya mwanamke mwenye kuugua Polycystic ovarian syndrome, kuliko wanawake wenye afya ya kawaida.

 

Watafiti Wairani wamegundia proteni inayochangia kuwepo utasa

Katika upande mwingine imbebainika kuwa, miongoni mwa wanawake wenye afya bora, proteini hii ya Apolipoprotein A1 huwepo kwa viwango mbali mbali lakini wakati mfuko wa uzazi unapokuwa tayari kupokea kijusi kiwango hicho hushuka kabisa na hivyo kumuwezesha mwanamke kushika mimba.

Kwa kufanyika uchunguzi zaidi, kunaweza kupatikana njia za kuangamiza proteini hiyo na hivyo kupelekea kuwepo uwezekano wa kukabiliana na moja ya sababu za utasa.

Hivi karibuni pia watafiti wa Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani walifanikiwa kugundua proteini ambayo huchangia katika kuenea na kusambaa seluli za saratani au uvimbe kwenye mayai ya mwanamke (ovary). Kwa kutumia fungomwili au antibody mpya, proteini hii hufungwa na hivyo kusitisha kasi ya kuenea saratani au uvimbe sambmba na kusimamisha kikamilifu Metastasis yaani ueneaji seluli za saratani.

Wanasayansi wamegundia proteini ambayo hueneza saratani kwenye mayai ya mwanamke

Watafiti wanaamini kuwa uvumbuzi huu utapelekea kutibu au kuzuia saratani ya mayai ya mwanamke.

Kwingineko mtafiti Muirani katika Chuo Kikuu cha Semnan kaskazini-kati mwa Iran kwa kutumia  carbon nanotubes amefanikiwa kuunda Polymer nanocomposites (PNC) ambazo  zina uwezo wa kurejea katika hali ya asili hata baada ya kubadilika muundo kwa sababu mbali mbali.  PNC hizo aghalabu hutumika katika sekta ya utengenezaji magari na pia katika sekta ya usafiri wa anga. Mada zinazotumika ni zile ambazo hata zikiwa katika mazingira ya joto kali au hata moto na hivyo kubadilika muundo huweza kurejea katika hali ya kawaida baada ya joto hilo kuondoka. Moja ya faida za teknolojia hii katika sekta ya viwanda vya magari ni kuwa, kwa mfano iwapo steering au bumper ya gari itabondeka wakati wa ajali inaweza kurejeshwa katika hali yake ya awali kwa kukarabatiwa pasina kuhitajia kubadilishwa.

Watafiti Wairani waunda mada imara ya bumber za magari

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azadi nchini Iran wamefanya utafiti katika maabara na kuzalisha vitambaa vya pamba ambavyo vina uwezo mkubwa wa kutobadilika rangi kutokana na miale ya jua. Aidha vitambaa hivyo vina uwezo wa kujisafisha na vinaweza kukabiliana na bakteria au vijidudu haribifu kwa mwili. Aidha kitambaa hicho kina uwezo wa kuzuia maji na hata mafuta kujipenyeza.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azadi Iran wameunda kitambaa chenye kustahamilki miale ya jua na chenye kujisafisha

Kwa kuzingatia utumizi mwingi wa vitambaa vya pamba, na pia kwa kuzingatia kutokuwepo sumu katika mada za Zirconium oxide nanoparticles ambazo zimetumika kutengeneza kitambaa hicho, kinaweza kutumika katika mahospitali na pia katika maeneo ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kutokea moto.

Kwingineko watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kemikali na Uhandisi wa Kemikali Iran mwaka 2016 walifanikiwa kuzalisha hapa nchini mada ambayo ni muhimu katika utengenezaji dawa za kutibu saratani inayojulikana kama Carboplatin.

Lengo la kuhakikisha Iran inajitengenezea mada hii ni kupungza gharama za matibabu ya waliougua saratani.

Carboplatin ni dawa aina ya antineoplastic ambayo ina uwezo wa kutibu anuai za saratani za mapafu, kibofu n.k.

Hadi sasa ni nchi chache sana duniani zenye uwezo wa kuzalisha mada hiyo yenye umuhimu mkubwa katika kutibu saratani. Kila mwaka takribani kilo 5 hadi 8 za dawa ya kutibu saratani ya cabrboplatin imekuwa ikiingizwa Iran kutoka nchi za kigeni. Kwa hivyo baada ya mafanikio ya wanasayansi wa Iran katika kutengeneza dawa hiyo, nchi hii itaweza kupunguza gharama za ununuzi wa dawa hiyo na hivyo matibabu ya saratani yatawezekana kwa bei nafuu zaidi.

Wanasayansi Wairani wamefanikiwa kuunda mada ya kutengeneza dawa ya saratani ya Carboplatin