Apr 02, 2017 08:02 UTC
  • Jumapili April Pili

Leo ni Jumapili tarehe 4 Rajab mwaka 1438 Hijria, sawa na Aprili Pili 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 846 iliyopita, alifariki dunia malenga wa Kiislamu Muhammad Ibn 'Ali al-Wasiti maarufu kwa jina la Ibn Muallim. Ibn Muallim alizaliwa mwaka 501 Hijiria. Mashairi ya malenga huyo yalibeba ujumbe wa maadili na tabia njema na masuala mengine yahusuyo jamii huku mengine yakihusiana na irfani. Athari pekee ya Ibn Muallim ni kitabu cha tungo za mashairi ya malenga huyo.

Ali al-Wasiti

Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, alizaliwa Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa hadithi maarufu za watoto nchini Denmark. Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na mtengeneza viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga hadithi na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1830 Miladia.

Hans Christian Andersen

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, alifariki dunia Samuel Morse mvumbuzi wa Marekani na mwanzilishi wa simu ya upepo (telegrafu.) Morse alizaliwa tarehe 27 April mwaka 1791 katika jimbo la Massachusetts nchini Marekani. Akiwa kijana alipendelea sana uchoraji na kwa miaka kadhaa alijihusisha na kazi hiyo. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana mwaka 1826 akaasisi akademia ya kimataifa ya sanaa za mkono. Mwaka 1832 aliteuliwa kuwa mwalimu wa uchoraji katika Chuo Kikuu cha New York. Katika kipindi hicho, Samuel Morse alianza kazi za umeme na  akafanya majaribio kadhaa katika uwanja huo. Baada ya hapo alifikia natija kwamba, wakati wowote umeme unapokuwa katika waya, unaweza kusafirisha habari kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Pamoja na hayo Morse hakuweza kufikia malengo tarajiwa na hivyo akaamua kumshirikisha Joseph Henry, mwanafizikia mwingine wa Marekani na kwa kutumia tajiriba na uzoefu wa msomi huyo alifanikiwa kuvumbua simu hiyo ya upepo.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, vikosi vya Jeshi la Majini vya Argentina vilivamia visiwa vya Falkland (Malvinas) na kuvikalia visiwa hivyo vya kiistratejia vilivyoko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Visiwa vya Falkland ambavyo Waargentina vinaviita Malvinas, viligunduliwa katika karne ya 16 na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza mwaka 1832. 

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, vibaraka wa utawala wa Baath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein walivamia na kuvunjia heshima Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib A.S katika mji mtakatifu wa Najaf na ya Imam Hussein A.S huko katika mji mtukufu wa Karbala, sambamba na kuyakandamiza mapambano ya Waislamu wa kusini mwa Iraq. Wananchi wa Iraq walianzisha mapambano ya kuuondoa madarakani utawala wa kidikteta Saddam Hussein baada ya muungano wa vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa kutekeleza oparesheni ya kuwaondoa wanajeshi wa Iraq katika ardhi ya Kuwait na kufuatia kushindwa kwa jeshi la Saddam Hussein. Wakati huo wanajeshi wa Marekani walisitisha oparesheni zao za kijeshi na kuungana na wanajeshi wa Saddam ili kumwaga damu za Wairaqi waliokuwa wakiendesha mapambano huku wakiwa kwenye saumu.

تعرض رژیم بعث عراق به اماکن مقدسه دو شهر نجف و اکربلا

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, aliaga dunia Papa John Paul wa Pili aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Papa John Paul wa Pili alizaliwa mwaka 1920 huko Poland na kufikia daraja ya uchungaji baada ya kuhitimu masomo ya dini. Mwaka 1964 Papa John Paul alikuwa askofu wa mji wa Kraku huko Poland na miaka mitatu baadaye akawa Kadinali. Hatimaye mwaka 1978 John Paul wa Pili aliteuliwa kushika wadhifa wa ngazi ya juu zaidi wa kanisa Katoliki, yaani Papa. 

Papa John Paul wa Pili

 

Tags