Apr 26, 2017 12:47 UTC
  • Jumatano tarehe 26 Aprili, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 28 Rajab 1438 Hijria sawa na 26 Aprili 2017.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as), ulianza safari yake kutoka mjini Madina. Hatua hiyo ilitanguliwa na kuaga dunia Muawia bin Abi Sufiyan hapo tarehe 15 ya mwezi huo huo wa Rajab na kuchukua mahala pale mwanaye, Yazid bin Muawiya. Yazidi alimtaka mtawala wa Madina kumlazimisha Imam Hussein ili atoe baia kwa ajili yake na endapo angekataa, basi amuue. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa Imam Hussein alikuwa akifahamu vyema kuwa Yazidi ni muovu na fasiki, alikataa kutoa baia hiyo na hivyo akaamua kuondoka mjini Madina kuelekea Makka, akiwa na watu wa familia ya Mtume na idadi kadhaa ya wafuasi wake.

Tarehe 26 Aprili miaka 412 iliyopita lilichapishwa gazeti la kwanza kabisa duniani nchini Ufaransa. Mhariri mkuu wa gazeti hilo lililopewa jina la Relation alikuwa Johann Carolus. gazeti hilo liliendelea kuchapishwa kwa kipindi cha miaka 70. Hii leo maelfu ya magazeti huchapishwa kila siku katika pembe mbalimbali za dunia na Wajapan wanahesabiwa kuwa wasomaji wakubwa zaidi wa magazeti kuliko watu wa maeneo mengine ya dunia.

Gazeti la Relation

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, sawa na tarehe 28 Rajab mwaka 1337 Hijria, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa Kiirani. Allamah Yazdi alijipatia elimu yake ya kidini nchini na huko Najaf nchini Iraq, kutoka kwa maulamaa kadhaa mashuhuri akiwemo Mirza Shirazi na kufikia daraja ya Ijtihad. Msomi huyo aliandika vitabu vingi, kikiwemo kitabu cha 'al U'rwatul Wuthqa.

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Ordibehesht 1315 Hijria Shamsia, kituo cha kwanza cha matangazo ya redio na telegrafu kilianza kazi nchini Iran. Mwanzoni mwa kuanzishwa kwake, kituo hicho kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Vita. Miaka iliyofuata vituo vya kurusha matangazo ya redio na telegrafu vilianzishwa katika miji mbalimbali ya Iran na idara hiyo ikakabidhiwa kwa Wizara ya Posta na Telegrafu.

Uzinduzi wa kituo cha kwanza cha matangazo, Iran

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa baada ya nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar kuungana. Kabla ya kuungana huko Tanganyika na Zanzibar zilikuwa zikikoloniwa na nchi mbalimbali ambapo nchi mkoloni wa mwisho ilikuwa Uingereza. Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1961 na Zanzibar mwaka 1963 baada ya mapambano ya wananchi ya kupigania uhuru dhidi ya mkoloni Muingereza. Julius Kambarage Nyerere alitoa wito wa kuungana Tanganyika na Zanzibar na ilipofika tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 1964 nchi mbili hizo ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tanzania iko mashariki mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Hindi huku ikipakana na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji.

Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Siku kama ya leo 31 iliyopita, kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine ambacho kilikuwa kikidhamini sehemu kubwa ya nishati ya umeme ya nchi hiyo kiliripuka na kusambaza mada hatari za miale ya radioactive. Awali Russia ilikadhibisha habari ya kutokea mlipuko katika kituo hicho. Hata hivyo baadaye ililazimika kukiri kutokea mlipuko katika kituo hicho cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl baada ya wingu kubwa la nyuklia lililosababishwa na mada za radioactive kuoneka waziwazi katika kituo hicho. Kasoro za kiufundi zilitajwa kuwa chanzo cha mlipuko huo. Katika tukio hilo, makumi ya maelfu ya watu waliathirika kwa namna tofauti ikiwemo kuongezeka maradhi mbalimbali. Mwaka 2000 Ukraine ilikifunga kabisa kituo cha nyuklia cha Chernobyl.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita mwafaka na tarehe 26 Aprili mwaka 1996, mashambulizi ya kijeshi ya siku 16 ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon kwa jina la "Vishada vya Hasira" yalimalizika. Katika operesheni hiyo jeshi la utawala wa Israel lilifanya mashambulio ya nchi kavu, anga na baharini huko kusini na hata katika ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mbali na kuharibu maeneo mengi ya raia na miundo mbinu na taasisi za kiuchumi, utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi raia 180 wa Lebanon na kujeruhi mamia ya wengine.

 

Tags