Jun 04, 2017 06:45 UTC
  • Jumapili, Juni 4, 2017

Leo ni Jumapili tarehe Tisa Ramadhani 1438 Hijria sawa na tarehe Nne Juni, 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, alifariki dunia Ruhullah Musawi Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuishi humu duniani kwa miaka 87. Baada ya kutangazwa habari ya kufariki kwake, ilimwengu wa Kiislamu uligubikwa na wingu la simanzi na huzuni. Imam Khomeini alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1902 huko katika mji wa Khomein katikati mwa Iran. Alianza harakati zake za kisiasa sambamba na shughuli za kielimu na kiutamaduni. Kutokana na shughuli zake za kisiasa zilizokuwa zikiukera sana utawala wa kidhalimu wa mfalme Shah, utawala huo ulimbaidisha Imam katika nchi za Uuruki na kisha Iraq. Katika kipindi cha miaka 13 akiwa uhamishoni huko Iraq, Imam (MA) alilea na kuwafunza wanafunzi wengi na wakati huohuo kufichua maovu yaliyokuwa yakifanywa humu nchini na utawala wa Shah kwa ushirikiano wa karibu wa Marekani. Baada ya kupamba moto mapambano na harakati za Kiislamu zilizokuwa zikiongozwa na Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah, hatimaye Imam alilazimika kutoka nchini Iraq na kuhamia Ufaransa, hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipofikia ushindi hapa nchini hapo mwaka 1979. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran.

Imam Ruhullah Musawi Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Baraza Linalomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mfumo wa Kiislamu wa Iran lilimchagua Sayyid Ali Khamenei, kuuongoza mfumo huu. Muda mfupi baada ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA), baraza hilo lilikutana kwa lengo la kumchagua mrithi wake. Wanachama wa baraza hilo ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi, walichunguza uzeofu wa kimapinduzi na sifa nyingine muhimu za Ayatollah Khamenei zikiwemo za ushujaa, uwezo mkubwa wa kuchambua mambo ya zama, ujuzi mkubwa wa masuala ya kidini, fikhi na sheria ya Kiislamu, uadilifu, utawala bora na kisha kumchagua kwa wingi wa kura kuwa Kiongozi Mkuu wa mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Leo ni tarehe nne Juni, siku muhimu katika kalenda ya dunia ambayo inafahamika kama siku ya kuwaunga mkono watoto kutokana na mashambulizi na ukatili. Mwaka 1982 na katika kuchunguza hali ya watoto wa Palestina na Lebanon ambao ni wahanga wakubwa wa mashambulizi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, tarehe nne ya kila mwaka ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa siku ya watoto wasio na hatia wahanga wa ukatili yaani ‘International Day of Innocent Chindren Victims of Aggression’ ambapo katika siku hiyo huchunguzwa machungu ya watoto wahanga wa ukandamizaji wa kimwili na kisaikolojia. Inafaa kuashiria hapa kwamba, hadi sasa karibu watoto laki mbili na elfu 50 duniani, wanatumikishwa kama askari katika migogoro mbalimbali. Akthari ya watoto hao hujiunga na makundi ya wabeba silaha kutokana na umasikini wa kupindukia. Aidha karibu nusu ya watu milioni 50 ambao wamelazimika kuwa wakimbizi duniani, ni watoto. Mbali na hayo ni kwamba, kati ya wakimbizi milioni 22 ambao wanasimamiwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), milioni 10 ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18. Kadhalika mamia ya watoto wanashikiliwa katika jela za kutisha za utawala haramu wa Kizayuni, huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

International Day of Innocent Chindren Victims of Aggression

Siku kama ya leo miaka 585 iliyopita, alifariki dunia Ologh Beig, msomi mkubwa wa elimu ya nyota wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 796 Hijiria eneo la Soltaniyeh, moja ya miji ya magharibi mwa Iran na kulelewa katika taasisi ya babu yake, Timur ambayo ni moja ya silsila ya utawala wa Timur. Akiwa na umri wa miaka 16 aliteuliwa kuwa kamanda wa jeshi katika mji wa Mā warāʼ al-Nahr (Transoxiana), mji wa katikati mwa Asia. Kinyume na utawala wa Timur, yeye hakupendelea kupanua dola hilo na badala yake akajikita katika utafiti na utalii. Katika kipindi hicho aliasisi kituo cha kielimu ambacho kilitoa elimu ya nyota. Aidha hatua yake nyingine ilikuwa ni kujenga kituoa cha kufuatilia nyota huko katika mji wa Samarqand hapo mwaka 828 Hijiria, ambacho kilitoa wasomi wengi wa masuala ya nyota.

Ologh Beig,

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 52, Alexis Claude Clairaut, mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Akiwa kijana mdogo alikuwa na maandalizi ya hali ya juu ya kielimu kiasi kwamba akiwa na miaka 10 tayari alikuwa amekuwa na uhodari katika masuala ya hesabati. Alipotimiza miaka 13 aliandika makala muhimu kuhusiana na hesabati. Aidha  alipotimiza umri wa miaka 16 Alexis Claude Clairaut aliandika makala mengine katika uwanja huo ambayo yaliwashangaza wasomi wengi wa hesabati wa zama hizo. Utunzi wake huo ulimfanya kuteuliwa kujiunga na chuo kikuu akiwa na umri mdogo ambapo aliendeleza utafiti wake uliozaa matunda katika uga huo.

Alexis Claude Clairaut

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, serikali ya China ilishambulia na kuwaua wanachuo wengi katika uwanja wa Tiananmen huko Peking mji mkuu wa nchi hiyo. Siku hiyo na licha ya kuwepo onyo la serikali dhidi ya kufanyika maandamano hayo, lakini maelfu ya wanachuo walikusanyika katika uwanja huo ili kuishinikiza serikali iruhusu kuwepo uhuru wa shughuli za kisiasa, kupunguzwa uwezo wa chama cha kikomonisti, kuongezwa uwezo wa bunge na kuchaguliwa wabunge na wananchi moja kwa moja. Baada ya kuona kuwa maandamano ya wanachuo hao yalikuwa yanaongezeka badala ya kupungua, polisi na jeshi la China liliamua kuyavunja kwa nguvu kwa kuua na kuwakandamiza wanachuo hao.

Shambulizi la Tiananmen