Jun 16, 2017 04:21 UTC
  • Ijumaa 16 Juni, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Ramadhani 1438 Hijria, sawa na 16 Juni, 2017

Siku kama ya leo miaka 1398 iliyopita Ali bin Abi Talib (as) Khalifa wa baada ya Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume alikufa shahidi. Siku mbili kabla ya hapo Imam Ali (as) alielekea msikitini kwa ajili ya Sala ya asubuhi na akiwa katika sijda alipigwa upanga kichwani na Ibn Muljim aliyekuwa mfuasi wa tapo la Khawarij na kumpasua utosini. Imam Ali (as) alikufa shahidi katika siku kama ya leo na hivyo kufikia saada aliyokuwa akiitaraji daima, yaani kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kuuliwa shahidi Imam Ali (as) kulisababisha pigo na msiba usioweza kusahaulika na kufutika kwa Uislamu na Waislamu.

Tarehe 21 Ramadhani miaka 334 iliyopita alifariki dunia faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabar Amili nchini Lebanon. Alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa kufanya uchunguzi mkubwa. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi vya fiqhi na hadithi na miongoni mwao ni kile cha Wasaailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika duru za elimu ya fiqhi. Baadhi ya vitabu vya msomi huyo mtajika ni al Jawahiru Saniyyah, Ahwalu Sahaba na al Ijazaat. 

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo. Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Aidha mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri. Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6. Mwanake huyo alitua katika orbiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia. Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo. Katika muda wa masaa 70 na dakika 50 aliyokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48.

Valentina Tereshkova

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu. Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu. Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Mapambano ya watu wa Soweto, Afrika Kusini

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil-udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani, aalimu na marjaa mkubwa wa Kiislamu baada ya kuugua. Allamah Fadhil Lankarani alizaliwa mnamo mwaka 1310 Hijria Shamsia katika mji wa kidini wa Qum huko kusini mwa Tehran na kuanza kujifunza masomo ya dini akiwa kijana mdogo. Aidha alipata kustafidi na mafunzo ya walimu wakubwa wa zama zake kama vile Ayatullahil udhma Burujerdi na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu awarehemu. Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani katika kipindi kifupi aliweza kufikia daraja ya ijtihad.

Ayatullahil-udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani

 

Tags