Jun 25, 2017 02:26 UTC
  • Jumapili, 25 Juni, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 30 Ramadhani mwaka 1438 Hijria, inayosadifiana na tarehe 25 Juni mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Kiafrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kundi hilo la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika wakarejea huko Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia.

Bendera ya Liberia

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, kufuatia harakati za kichokozi za Marekani katika eneo la Peninsula ya Korea, Korea Kaskazini iliishambulia Korea Kusini na kusonga mbele haraka upande wa nchi hiyo hasimu. Hata hivyo kupasishwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi nyingine 15 zilituma askari wao kwa ajili ya kukabiliana na kuzuia kusonga mbele zaidi Korea Kaskazini sambamba na kuisaidia Korea Kusini. Hatimaye majeshi hayo ya kigeni kwa kushirikiana na Korea Kusini yaliweza kuizuia kusonga mbele Korea Kaskazini. Hata hivyo hatua ya China ya kuingilia kati vita hivyo kwa maslahi ya Pyongyang, kulifanya uvamizi wa Marekani na vikosi vya kigeni kufikia tamati katika eneo hilo. Ni baada ya hapo ndipo kukaanza mchakato wa mazungumzo ambapo mwaka 1953 kulitiwa saini makubaliano ya usitishaji vita hivyo. Hata hivyo hadi sasa mkataba rasmi wa amani baina ya Korea mbili bado haujatiwa saini na daima hali ya ushindani imeendelea kushuhudiwa baina yao, huku Marekani ikiendeleza siasa zake za uchochezi katika eneo hilo.

Mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea, Korea Kaskazini

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita baada ya kutiwa mbaroni Imamu Khomein (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Shirika la Intelijinsia na Usalama wa Taifa la Iran wakati huo, maarufu kwa jina la SAVAK, alihamishiwa katika kambi ya Eshratabad. Siku 40 baada ya kuzuiliwa katika kambi hiyo, Imamu kwanza alibaidishwa katika nchi ya Uturuki na mwaka mmoja baadaye akabaidishiwa tena nchini Iraq. Kwa kipindi cha miaka 13 Imamu Khomein aliendeleza harakati za mapinduzi kupitia wanafunzi wake. Katika kipindi hicho, wanafunzi hao walikuwa wakifanya mawasiliano na watu wa Iran na kuwafikishia ujumbe kutoka kwake. Imamu alirejea nchini Iran, mwezi Bahman mwaka 1357 sawa na Februari mwaka 1979 Miladia na kuanguka rasmi utawala wa kifalme wa Shah siku 10 tangu aliporejea nchini Imam (MA).

Nembo ya SAVAK

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru wake. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao.

Bendera ya Msumbiji

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, kwa mara nyingine ndege za utawala vamizi wa Saddam na katika siku za mwisho za vita vya kulazimishwa vya miaka minane dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zilishambulia kwa mabomu ya silaha za kemikali kisiwa cha Majnoon. Katika hujuma hiyo ya kinyama, mamia ya wapiganaji wa Iran ya Kiislamu waliuawa shahidi. Tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, utawala huo wa zamani wa Iraq, ulikuwa ukitumia silaha hizo zilizopigwa marufuku kimataifa kwa lengo la kuilazimisha Tehran isalimu amri. Kiasi kwamba kwa kipindi cha miaka minane, jeshi la Iraq lilikuwa limetumia silaha hizo mara 200 ambapo kutokana na silaha hizo karibu askari na raia wa kawaida 30,000 wa Iran waliuawa shahidi au kujeruhiwa. Madola ya Magharibi ambayo yalikuwa yakiipatia Iraq silaha hizo, hayakuichukulia hatua yoyote serikali ya wakati huo ya Baghdad bali yaliendelea kusalia kimya kuhusiana na suala hilo.

Moshi wa mabomu ya kemikali

 

 

Tags