Mar 15, 2016 05:01 UTC
  • Jumanne, Machi 15, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1437 Hijria sawa na tarehe 15 Machi 2016 Milaadia.

Siku kama hii ya leo miaka 27 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.

Miaka 28 iliyopita utawala wa zamani wa Iraq wa Baath uliushambulia mji wa Wakurdi wa Halabcha huko kaskazini mashariki mwa Iraq. Makumi ya ndege za kivita za utawala wa Saddam Hussein zilifanya mashambulizi ya kinyama kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Kikurdi wa mji wa Halabcha. Utawala wa Baath ulianzisha mashambulizi hayo katika hali ambayo kwa upande mmoja utawala huo ulikuwa umeshindwa kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa Iran na wa Kikurdi wa Iraq na kwa upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabcha waliwakaribisha na kuwaunga mkono wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo waliokuwa wakifanyiwa na Saddam Hussein. Nchi za Magharibi ambazo ndizo zilizoupatia utawala wa Saddam teknolojia na nyenzo zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa silaha hizo za kemikali, hazikuchukua hatua yoyote ya kivitendo mbele ya jinai hizo za Saddam Hussein, licha ya karibu watu elfu tano kuuawa katika maafa hayo ya kutisha ya Halabcha.

Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia mwaka 1901.

Na miaka 765 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 5 Jamadithani mwaka 672 alifariki dunia Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulawi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Kunya ambao ni moja kati ya miji ya zamani ya Iran ulioko kusini mwa Uturuki ya leo. Maulawi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Maulawi alizaliwa mwaka 604 Hijria Shamsia katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya sasa na baada ya muda akahamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maulawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maualana na Rabaiyat.