Jumatano 2 Agosti, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 9 Dhulqaada 1438 Hijria sawa na Agosti Pili, 2017.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq, na kutoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala wa zamani wa Iraq kwa mara kadhaa ulitumia silaha za kemikali dhidi ya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pamoja na hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutoa azimio lolote dhidi ya utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Agosti 1934, alifariki dunia Jemadari Paul von Hindenburg, Rais wa zamani wa Ujerumani na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya majeshi ya nchi hiyo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Hindenburg alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Ujerumani mwaka 1925.

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, yaani tarehe Pili Agosti 1990, jeshi la utawala wa Ba'ath nchini Iraq lilivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Kuwait iliyoko kusini mwa Iraq. Hilo lilihesabiwa kuwa shambulio la pili na kuikalia kwa mabavu nchi jirani, baada ya kuishambulia na kuikalia kwa mabavu baadhi ya mikoa ya Iran mwaka 1980. Saddam Hussein alitangaza kuwa, Kuwait ni sehemu ya ardhi ya Iraq na kwamba ni jimbo la 19 la nchi hiyo.

Tarehe Pili Agosti miaka 95 iliyopita alifariki dunia Alexander Graham Bell mvumbuzi wa wa Kimarekani. Tangu akiwa kijana, Bell alivutiwa mno na masuala ya ufundi. Baada ya utafiti wa miaka kumi Alexander Graham Bell alifanikiwa kutengeneza chombo cha kuhamisha sauti ambacho kilikuwa mwanzo wa simu zinazotumiwa kwa sasa. Bell pia alifanikiwa kutengeneza chombo cha kunasa sauti cha phonograph. Graham Bell alifariki dunia mwaka 1922.

Na tarehe 11 Mordad 1288 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri mwanachuoni mkubwa ambae alikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Qajjar hapa nchini. Ayatullah Fadhlullah Nouri alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mapinduzi ya katiba, na hali kadhalika alisimama kidete katika kupinga sheria zilizopitishwa bungeni ambazo zilikuwa zikikinzana na mafundisho ya Uislamu.
