Sep 02, 2017 02:32 UTC
  • Jumamosi, Septemba Pili, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1438 Hijria sawa na tarehe Pili Septemba mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 216 iliyopita, baada ya vita kadhaa baina ya vikosi vya utawala wa Othmania na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja na vikosi vya Ufaransa kwa upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa katika vita na kulazimika kuondoka kikamilifu kutoka nchini Misri. Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleone Bonaparte kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa hasimu na mshindani mkuu wa Ufaransa katika masuala ya kiuchumi na kijeshi, iliona kuwa maslahi yake yapo hatarini. Ni kwa sababgu hiyo, ndio maana Uingereza ikaungana na utawala wa Othmania kwa shabaha ya kwenda kuitoa Ufaransa huko Misri na kuzuia jeshi la Ufaransa lisizidi kusonga mbele. ***

Misri

Katika siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu mahiri wa elimu ya fizikia wa Ireland alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1805 na alionyesha kuwa na akili mno na kipaji cha hali ya juu tangu akiwa mtoto mdogo. Hamilton alisoma kwa ami yake aliyekuwa kasisi. Alipofikisha umri wa mjiaka 13, mwanafizikia huyo mtajika wa Ireland alikuwa tayari anazifahamu lugha kadhaa za kimataifa. Hadi anafikisha umri wa miaka 22 alikuwa tayari ni mwalimu katika elimu ya nujumu. ***

William Rowan Hamilton

Miaka 94 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja alifariki dunia Ayatullah Mirza Jawad Maliki Tabrizi Ustadhi mkubwa wa Akhlaqi, msomi na Arif. Alizaliwa katika mji wa Tabriz moja ya miji ya Iran na baada ya kukamilisha masomo yake ya utangulizi na ya kati alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Akiwa huko alihudhuria darsa za Maustadhi mahiri katika zama hizo kama Haji Agha Reza Hamadani, Akhund Khorasani, Muhadith Nuri na Akhund Hamadani. Mwanzuoni huyo mbali na kufundisha na kulea wanafunzi wengi hakuwa nyuma pia katika taaluma ya uandishio wa vitabu. Asrar Salat, al-Muraqibaat na A'amal Sunna ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Mirza Jawad Maliki Tabrizi. ***

Ayatullah Mirza Jawad Maliki Tabrizi

Tarehe Pili Septemba 1945 yaani miaka 72 iliyopita nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19. Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. ***

Bendera ya Vietnam

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote. Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya Waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki. Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani Douglas MacArthur akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan. Mwaka 1951, nchi 49 duniani, zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe. ***

Kusalimu amri Japana na kufikia tamati Vita vya Pili vya Dunia

Na miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 7.3 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika eneo la Buin Zahra huko kaskazini magharibi mwa Iran. Mtetemeko huo mkubwa uliua zaidi ya watu elfu 20 na kujeruhi maelfu ya wengine. Mtetemeko huo wa ardhi ulitokea wakati wa usiku na hivyo kupelekea watu wachache tu kunusurika na janga hilo la kimaumbile. Aidha mtetemeko huo wa Buin Zahra uliharibu kabisa vijiji 120 na kusababisha hasara kubwa kwa mamia ya nyumba za eneo hilo. Baada tu ya mtetemeko huo wananchi wa Iran waliharakia kuwapelekea misaada wenzao wa Buin Zahra. ***

Tetemeko la ardhi katika mji wa Buin Zahra kaskazini magharibi mwa Iran