Oct 02, 2017 04:28 UTC
  • Jumatatu, Oktoba 2,  2017

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Muharram mwaka 1439 Hijiria sawa na tarehe 2 Oktoba mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (swa) ulianza harakati ya kuelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa kidhalimu wa Yazidi bin Muawiya baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura. Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake tarehe 10 mwaka 61 Hijria, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalipora mali na vitu vyote vya watu wa familia ya Mtume (saw). Askari hao sambamba na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as), watu wa familia ya Mtume na masahaba zake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao kama vidani na herini. Hatimaye jioni ya siku kama ya leo msafara wa mateka wa familia ya Mtume uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as), ulipelekwa Kufa nchini Iraq ukiwa njiani kuelekea Sham. Hatua hiyo ilifungua mapambano mengine ya kufichua na kuweka wazi uhalifu na ukatili wa kizazi cha Banii Umayyah.

Tarehe Pili Oktoba miaka 113 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Siku zote mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi ambapo baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Graham Greene

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1941, Adolph Hitler kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi alitoa amri ya kuanza kwa shambulizi la pili la jeshi la Ujerumani dhidi ya Urusi ya zamani. Kwenye vita vya kwanza dhidi ya Urusi vilivyoanza tarehe 22 Juni 1941, Ujerumani iliweza kuikalia kwa mabavu sehemu kadhaa za ardhi ya Urusi. Lengo la kufanywa shambulio hilo la Dikteta Hitler, lilikuwa ni kurahisisha operesheni za kijeshi, kudhoofisha nguvu za Jeshi Jekundu na kudhibiti ardhi zaidi za Urusi, na hasa Moscow mji mkuu wa nchi hiyo.

Adolph Hitler
کشور گینه

Na miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na ilipoanza karne ya 19, Wafaransa wakawa na satua zaidi nchini humo na ulipotimia mwaka 1849, nchi hiyo ikakoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Bendera ya Guinea Conakry