Nov 13, 2017 07:31 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 13

Hujambo mpenzi msikilizaji wa RT na hususan ashiki wa spoti na karibu tutupie jicho matukio mawili matatu ya michezo yaliyogonga vichwa vya habari ndani na nje ya nchi katika kipindi cha siku saba zilizopita, karibu..

Iran yaendelea kujinoa, yainyoa Panama

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeinyuka Panama mabao 2-1 katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki, ambao umetumiwa na vijana wa Team Melli kama wanavyojulikana hapa nchini, kupasha misulu moto kwa ajili ya Kombe la Dunia mwakani nchini Russia. Katika mtanange huo wa Alkhamisi jioni uliopigwa katika uwanja wa mji wa Graz, nchini Austria vijana wa Iran walipata bao la kwanza kupitia kiungo Ashkan Dejagah kwa njia ya penati kunako dakika ya 16. Dakika tatu baadaye hata kabla ya mate kukauka, mchezaji Saman Ghoddos aliongeza la pili na kuihakikishia timu hiyo ya Iran ushindi mnono. Bao la Panama la kufutia mchozi lilifungwa na mchezaji Gabriel Torres.  Mwezi Oktoba mwaka huu, timu hiyo ya taifa ya mpira wa miguu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliinyuka Togo mabao 2-0 katika mchuano mwingine wa kimataifa wa kirafiki, wa kujiandaa kwa ajili ya Kombe la Dunia mwakani. Aidha mwezi huo huo, iliilazimisha Russia sare ya bao 1-1 katika mechi nyingine ya kirafiki.

Timu ya Karate ya Iran yatwaa ubingwa Armenia

Timu ya taifa ya mchezo wa karate ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Armenia. Makarateka wa Iran wameibuka washindi baada ya kuzoa jumla ya medali 11 za dhahabu, sita za fedha na shaba saba, katika mashindano hayo yanayofahamika kama WSKF Shotokan Karate-do tournament. Wenyeji Armenia wameibuka katika nafasi ya pili huku Georgia ikifunga orodha ya tatu bora.

Mehdizadeh, karateka mashuhuri wa Iran

Wanakarate wa Kiirani waliotia kibindoni medali za dhahabu ni pamoja na Alireza Nadimi, Mehran Afkhami, Hadi Habibpour, Nader Gharaei, Mahsa Safi, Bahareh Bigdeli, Helia Kamasi, Atousa Golshadnejad, Anid Halvaei na Hossein Rivaz. Medali nyingine ya dhahabu ya Iran ilitwaliwa na timu ya wanakarate mabarobaro wa Junior Kata inayowajumuisha Mehran Afkhami, Hossein Pakrou na Alireza Nadimi.

Mbio: Wakenya wazidi kutamalaki mbio za Marathon

Mwanariadha nyota wa Kenya Ruth Chepng’etich siku ya Jumapili alidhihirisha kwamba yeye ni malkia wa jiji la Istanbul nchini Uturuki kwa kushinda mbio za marathon, miezi saba tu baada ya kutawazwa mshindi wa nusu-marathon. Mkenya huyo atazawadiwa Shilingi 5, 180,000 za Kenya sawa na Dola elfu 51 za Marekani, kwa kukata utepe kwa saa 2, dakika 22 na sekunde 36.

Nafasi ya pili ilinyakuliwa na Mkenya Visiline Jepkeshosaa 2, dakika 22 na sekunde 40, huku raia wa Ethiopia Haylay Letebrhan akafunga orodha ya tatu-bora (2:25:14). Katika kitengo cha wanaume, nafasi tatu za kwanza zilinyakuliwa na Mfaransa Abraham Kiprotich kwa kutumia saa 2, dakika 11 na sekunde 22, Mkenya Jacob Kendagor saa 2, dakika 11 na sekunde 27 na Muethiopia Bazu Worku saa 2, dakika 11 na sekunde 39. Huku hayo yakirifiwa, Wakenya Eliud Kipchoge na Mary Keitany waliibuka washindi wa mataji ya dunia ya wakimbiaji bora wa mbio za kilomita 42 za AIMS mwaka huu 2017. Ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Kipchoge kunyakua tuzo hii, ambayo mshindi anajulikana baada ya wanachama 435 kupiga kura kuhusu marathon za kifahari kutoka mataifa 114.

Kipchoge alishinda taji la Berlin Marathon nchini Ujerumani kwa saa 2, dakika 3 na sekunde 32 mwezi Septemba mwaka 2017, muda ambao ni kasi ya juu kushuhudiwa katika marathon mwaka huu. Itakumbukwa kuwa Kipchoge alitimka umbali wa kilomita 42 katika mbio za Breaking2 mjini Monza nchini Italia mwezi Mei kwa kutumia saa 2. Hafla ya kutuza washindi wa AIMS (Association of International Marathons and Distance Races) ilifanyika jijini Athens nchini Ugiriki Ijumaa ya Novemba 10. Keitany alipata ufanisi wa kuwa mshindi wa AIMS kwa kuweka rekodi mpya ya marathon ya wanawake ya saa 2, dakika 17 na sekunde 01 aliposhinda taji la London Marathon nchini Uingereza mwezi Aprili mwaka huu 2017. Mbali na hayo, mwanariadha chipukizi mwenye umri wa miaka 23 Samuel Kalalei aliongoza Wakenya wawili kutamalaki mbio za Athen Classic Marathon siku ya Jumapili. Kalalei alibuka kidedea kwa kutumia saa mbili, dakika 12 na sekunde 17, mbele ya Wakenya Milton Kiplagat Rotich na Jonathan Kiptoo Yego. Hata hivyo katika safu ya wanawake, Mhabeshi Bedaru Hirpa Badane aliibuka mshindi kwa kutumia saa mbili, dakika 34 na sekunde 18.

Senegal, Morocco na Tunisia zatinga Kombe la Dunia

Nchi tano zimejitakia tiketi ya kuliwakilisha bara Afrika katika fainali za Kombe la Dunia mwaka ujao 2018 nchini Russia. Senegal maarufu kama Simba wa Teranga wamefuzu kwa fainali hizo kwa mara ya pili baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Afrika Kusini katika uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane siku ya Ijumaa. Watarejea Urusi kucheza miaka 16 baada yao kushangaza watu wakicheza katika Kombe la Dunia mara ya kwanza, michuano iliyoandaliwa Korea Kusini na Japan. Sadio Mane, alirerejea mapema kutoka kuuguza jeraha, alichangia sana ushindi huo wa Simba wa Teranga. Alitoa pasi safi kwa mshambuliaji wa West Ham Diafra Sakho aliyeweza kumbwaga kipa wa Bafana Bafana Itumeleng Khune, na kuwaweka Senegal kifua mbele katika mechi hiyo dakika ya 12. Winga huyo wa Liverpool kisha alisaidia kushinda mechi hiyo kwa kuchangia bao la pili dakika mbili kabla ya muda wa mapumziko.

Nchi 5 za Afrika ni miongoni mwa mataifa yatakayoshiriki Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Russia

Timu zote mbili zitakutana tena Dakar Jumanne katika mechi ambayo itakuwa tu ya kutimiza wajibu kwani Senegal wamejiunga na Nigeria na Misri katika orodha ya nchi ambazo zimefuzu Kombe la Dunia. Morocco na Tunisia ni timu nyingine zitakazoliwakilisha bara Afrika nchini Russia mwakani. Tunisia walihitaji alama moja tu ili kwenda kushiriki michuano hiyo na wamefanikiwa kupata alama moja baada ya kulazimisha suluhu ya bila kufungana dhidi ya timu ya taifa ya Libya. Suluhu hiyo imewafanya vijana hao wa Kiarabu kufikisha idadi ya alama 14, alama ambazo DR Kongo wameshindwa kuzifikia huku leo wakilazimishwa suluhu ya bao moja kwa moja dhidi ya timu ya taifa ya Guinea. Morocco kwa upande wao wamekata tiketi kuelekea Kombe la Dunia baada ya kuwachabanga Ivory Coast kwa jumla ya mabao mawili kwa nunge katika mchezo uliokuwa wa kuamua nani wakwenda kombe la dunia kutoka kutoka Kundi C. Alianza Nabir Dirar dakika ya 25 kuwapa wageni bao la kuongoza. Wakati Ivory Coast wakijipanga kusawazisha dakika 5 baadaye Mehdi Benatia aliwapa wageni bao la pili lililowahakikishia tiketi kuelekea Urusi.  Kwa matokeo hayo sasa yanaifanya Afrika kukamilisha idadi ya washiriki 5 katika kombe la dunia ambao ni Misri, Nigeria, Senegal, Tunisia na Morocco.

Tanzania yailazimisha Benin 1-1

Na nikudokeze tu kwamba, timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars imewalazimisha sare ya 1-1 wenyeji Benin katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Jumapili katika wa Uwanja wa l'Amitie mjini Cotonou. Bao la Taifa lilifungwa na kiungo Elias Maguri aliyefunga akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya.

…………………………TAMATI….………………