Nov 17, 2017 02:43 UTC
  • Ijumaa, Novemba 17, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Mfunguo Tano Safar 1439 Hijria, sawa na Novemba 17, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1428 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63. Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake, ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.

رحلت پیامبر اکرم (ص)

Miaka 1389 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka wa 50 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake. Mjukuu huyo wa Mtume aliuawa shahidi kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, mfereji wa Suez ambao unauinganisha Bahari ya Mediterranian na Bahari Nyekundu ulifunguliwa. Mfereji huo wenye urefu wa kilometa 167 na upana wa mita 120 hadi 200 ulichimbwa chini ya usimamizi wa mhandisi wa Ufaransa, Ferdinand de Lesseps. Mfereji wa Suezi pia unahesabiwa kuwa ni mpaka kati ya bara la Asia na bara la Afrika.

Ferdinand de Lesseps

Miaka 267 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 17 Novemba 1750, alizaliwa Nicolas Appert mwanasayansi wa Ufaransa. Appert aligundua njia ya kuhifadhi chakula kwa kuondoa vijidudu au Pasteurization, ambayo ilileta mabadiliko makubwa katika kuvihifadhi vyakula ili visioze. Nicolas Appert aliaga dunia mwaka 1841 kutokana na kusakamwa na umasikini.

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita yaani tarehe 17 Novemba mwaka 1982, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein. Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath. Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.

 

Tags