Mar 25, 2016 00:50 UTC
  • Ijumaa, Machi 25, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 15 Mfunguo Tisa Jumadi Thani 1437 Hijria sawa na 25 Machi 2016 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilianza vita vya Jamal, baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.

Tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 666 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.

Tarehe 25 Machi miaka 41 iliyopita Mfalme wa wakati huo wa Saudi Arabia, Faisal bin Abdulaziz, aliuawa na mwana wa ndugu yake mwenyewe, Faisal bin Saaid bin Abdulaziz. Faisal bin Saaid alifanya mauaji hayo akilalamikia kupunguzwa kwa mshahara wake. Japokuwa hitilafu katika kizazi cha wafalme wa Saudi Arabia zimekuwepo siku zote na zimekuwa zikipamba moto mara kwa mara lakini mauaji ya Mfalme Faisal yalikuwa ya kwanza ya mfalme wa nchi hiyo kutokana na hitilafu kama hizo. Muuaji wa Mfalme Faisal pia alikatwa kichwa mbele ya umati wa watu tarehe 18 Juni mwaka 1975. Baada ya Faisal, Khalid mwana mwingine wa Abdulaziz alishika kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.

Siku kama hii ya leo miaka 22 iliyopita, vikosi vamizi vya Marekani ambavyo mwezi Disemba 1992 viliwasili nchini Somalia kwa kisingizio eti cha kukomesha uasi nchini humo, hatimaye vililazimika kuondoka katika nchi hiyo baada ya kushindwa vibaya bila ya kutarajia. Mwaka 1991 makundi mbalimbali ya Somalia yalimpindua dikteta wa nchi hiyo Muhammad Siad Barre. Hata hivyo makundi hayo yalishindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na mkwamo huo wa kisiasa ukapelekea kuzuka vita vya ndani nchini humo. Marekani ilituma wanajeshi wake huko Somalia katika fremu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kulinda maslahi yake nchini humo, kutokana na nafasi muhimu ya Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika. Askari wa Marekani walikabiliwa na mapambano makali ya Wasomali na kupoteza askari karibu 100.

Na miaka 59 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo mkataba wa kuasisi Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya au kwa jina jingine Soko la Pamoja la Ulaya ulisainiwa huko Roma mji mkuu wa Italia kati ya wawakilishi wa nchi mbalimbali za bara hilo. Jumuiya hiyo iliundwa kwa lengo la kuasisi umoja wa forodha kati ya nchi wanachama ili kufuta ushuru wa bidhaa na baada ya hapo, ubadilishanaji wa bidhaa, nguvu kazi, vitega uchumi na huduma nyinginezo pia ukawa huru kati ya nchi wanachama. Jumuiya hiyo ilikuwa utangulizi wa kuundwa Umoja wa Ulaya mwaka 1992.