Dec 27, 2017 02:40 UTC
  • Jumatano tarehe 27 Disemba, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 8 Rabiuthani, 1439 Hijria sawa na 27 Disemba, 2017

Siku kama ya leo miaka 1207 iliyopita alizaliwa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Askari alilazimishwa na watawala wa Bani Abbas kwenda uhamishoni huko Samurra akiwa pamoja na baba yake na kufaidika na elimu ya Imam Hadi kwa kipindi cha miaka 13. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha karibu miaka sita baada ya kuuawa shahidi baba yake. Sehemu ya umri wake wa miaka 28 uliishia katika jela za watawala madhalimu wa Bani Abbas au akiwa uhamishoni na chini ya udhibiti wa watawala hao. Hata hivyo mtukufu huyo hakuacha kueneza maarifa sahihi ya Uislamu na kulea kizazi cha wanazuoni hodari.

Katika siku kama ya leo miaka 1082 iliyopita yaani mwaka 357 Hijria, aliaga dunia Abu Feras al-Hamdani malenga na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Mbali na kuandika mashairi, Abu Feras al-Hamdani alikuwa mpiganaji na watu wa karibu wa Seif ad-Dawlah mtawala wa Halab na alikuwa miongoni mwa makamanda wake.

Abu Feras al-Hamdani

Miaka 195 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu.

Louis Pasteur

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulianzishwa. Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa. Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York Marekani.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, kufuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mkataba wa kihistoria ulitiwa saini mjini Moscow. Mkataba huo ulitiwa saini na wawakilishi wa nchi tatu za Uingereza, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, Peninsula ya Korea ambayo hadi katika zama hizo ilikuwa nchi moja ikagawanywa katika sehemu mbili. Kwa utaratibu huo, kukatokea nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Kusini mgawanyiko ambao ungalipo hadi leo.

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita Bi Benazir Bhutto kiongozi wa Chama cha Wananchi cha Pakistan (PPP) aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mlipuko wa bomu uliofanywa na magaidi huko Rawalpindi kaskazini mashariki mwa Pakistan. Mbali na Bi Benazir Bhutto, watu wengine karibu 20 wafuasi wa chama cha PPP waliuawa pia katika mlipuko huo. Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kuenguliwa madarakani serikali ya kijeshi iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Muhammad Zia ul Haq.

Benazir Bhutto

Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote katika Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa.

Mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Gaza

 

Tags