Feb 14, 2018 11:51 UTC
  • Jumatano tarehe 14 Februari 2018

Leo ni Jumatano tarehe 27 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 14 Februari 2018.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita Wazayuni waliokuwa na silaha wanachama wa kundi la kigaidi la Palmakh waliendeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Palestina kwa kutekeleza operesheni ya kigaidi dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sa'sa' huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika operesheni hiyo iliyoendelea hadi kesho yake nyumba 20 za raia wa Palestina ziliharibiwa na watu 60 waliokuwemo wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wakauawa kwa umati. Hadi miaka kadhaa iliyopita Wazayuni wa Kiyahudi walikuwa wakiyataja mauaji ya kinyama ya kijiji cha Sa'sa' kuwa ni mfano wa wazi wa kuangamizwa kwa umati Wapalestina.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, yaani sawa na tarehe 14 Februari mwaka 1945, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia nchi mbili za Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya Ujerumani. Ndege 1773 za kijeshi zilitumiwa katika mashambulizi hayo ambayo ndiyo yaliyokuwa na hasara kubwa zaidi ya mali na nafsi duniani hadi hii leo. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Marekani na Uingereza yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tatu yalisawazisha na ardhi miji kadhaa ya viwanda ya Ujerumani na kuifanya majivu matupu. Raia kati ya laki moja na nusu hadi laki mbili na nusu waliuawa kinyama katika mashambulizi hayo.

Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Martin Scott tabibu mpasuaji wa Uingereza alifanikiwa kuunganisha figo ya mwanadamu. Siku hiyo Prf. Scott alichukua figo ya mtu aliyekuwa amefariki dunia na kuiunganisha na mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika hospitali moja ya Leeds huko Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini alitoa fatuwa iliyomtambua Salman Rushdie, mwandishi wa kitabu cha "Aya za Shetani" au Satanic Verses kuwa ameritadi na kuondoka katika dini ya Kiislamu. Katika kitabu hicho Rushdie alimvunjia heshima na kudhalilisha Mtume Muhammad (saw), kitabu kitukufu cha Qur'ani na matukufu mengine ya Kiislamu. Uandishi na uchapishaji wa kitabu hicho ulifanyika kwa njama na msaada wa nchi za Magharibi. Hata hivyo fatuwa ya Imam Khomeini dhidi ya murtadi Salman Rushdie, iliwaamsha Waislamu na kuwatahadharisha kuhusu njama hiyo. Fatuwa hiyo ya Imam iliungwa mkono na waandishi wengi huru duniani, maulamaa wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC.

Murtadi Salman Rushdie

Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, aliuawa Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon kwenye mlipuko wa bomu lililotegwa garini huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Alikuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri nchini Lebanon na wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa miaka 61. Hariri alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Lebanon kutokea mwaka 1992, muda mfupi baada ya kumalizika vita vya ndani vya Lebanon hadi mwaka 1998, na kuchukua tena wadhifa huo mwaka 2000 hadi 2004. 

Rafiq Hariri

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, ilianza harakati ya kupigania uhuru ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kiimla wa Aal-Khalifah. Tangu Bahrain ilipopata uhuru mnamo mwaka 1971, wananchi wa nchi nchi hiyo wamekuwa wakitaka uhuru na demokrasia ambavyo vimekuwa vikikandamizwa na utawala huo. Tangu wakati huo, Waislamu wa Kishia ambao ndio wanaounda asilimia kubwa ya raia wa nchi hiyo, wamekuwa wakibaguliwa, kukandamizwa na kunyimwa haki zao za kimsingi. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana kwa mara kadhaa harakati hizo za kupigania uhuru zikawa zinaibuka dhidi ya utawala huo wa Aal-Khalifah ambao una mafungamano na Saudi Arabia ya Kiwahabi huku ukiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata hivyo badala ya utawala huo kusikiliza matakwa ya wananchi umekuwa ukitumia mtutu wa bunduki na ukandamizaji wa kuchupa mipaka katika kuzima harakati hizo.

Harakati ya kupigania uhuru ya watu wa Bahrain