Jumapili 18 Februari, 2018
Leo ni Jumapili tarehe Mosi Jamadi tha-Thani 1439 Hijiria, mwafaka na tarehe 18 Februari mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 454 iliyopita, Michel Angelo Buonarroti mchoraji, mchongaji wa sanamu, msanifu majengo na malenga mkubwa wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 89. Michel Angelo alizaliwa mwaka 1475 Miladia na kuanza kujishughulisha na uchoraji na kuchonga sanamu licha ya upinzani wa baba yake. Malenga huyo wa Kiitalia alionyesha kipaji chake haraka katika uwanja wa uchoraji, uchongaji sanamu na usanifu majengo. Uchongaji wa sanamu za Manabii Isa na Musa huko Italia ni moja kati ya kazi kuu za kisanaa zilizofanywa na Michel Angelo katika zama zake hizo.
Siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, ukoloni wa Ufaransa ambao ulianza tangu mwaka 1830 dhidi ya Algeria, ulishindwa vibaya na wapiganaji wa Amir Abdelkader al-Djezairi, kiasi kwamba theluthi moja ya askari wa Ufaransa waliuawa na nusu nyingine ya waliobakia hai wakiishia kukamatwa mateka. Wakati huo Wafaransa ambao ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kupata hasara kubwa ya namna hiyo barani Afrika, ili kukusanya nguvu waliamua kuomba suluhu. Hata hivyo Amir Abdelkader al-Djezairi alikataa ombi hilo, hadi baada ya kupita karibu miaka miwili na kuikomboa ardhi yote ya Algeria kutoka mikononi mwa Wafaransa hao wavamizi. Hata hivyo miaka kadhaa baadaye Ufaransa iliweza kuidhibiti tena nchi hiyo, baada ya kuongeza askari na zana za kijeshi sambamba na kuwatumia baadhi ya viongozi wahaini wa makabila ndani ya Algeria.
Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, askari wa Ufaransa na Uhispania, walivunja mapambano ya wanamapambano wa Morocco chini ya uongozi wa Abd el-Krim Rifi na kupelekea mtetezi huyo wa Kiislamu, kubaidishwa kusini mwa Afrika. Abd el-Krim Rifi alianzisha mapambano yake sambamba na kuanza uvamizi wa Uhispania katika sehemu ya ardhi ya Morocco hapo mwaka 1912 Miladia. Hata hivyo na licha ya mkoloni huyo kuwa na nguvu kubwa na kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Morocco wasio na hatia, mwaka 1921 wapiganaji wa Abd el-Krim Rifi walipata ushindi mkubwa kiasi cha kuyafanya baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kutangaza Jamhuri. Katika hali hiyo Wafaransa nao ambao walikuwa wakiyadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo walipatwa na hofu kufuatia ushindi wa wananchi dhidi ya Wahispania na kwa ajili hiyo mwanzoni mwa mwaka 1924 wakaanzisha hujuma kubwa dhidi ya wanamapambano hao. Jeshi la Ufaransa chini ya Jemadari Philippe Pétain hata kama mwanzoni lilishindwa vibaya na wanamuqawama wa Morocco, lakini mwezi Februari 1926 katika siku kama ya leo liliwashinda wapiganaji wa Abd el-Krim Rifi baada ya kupata msaada wa kijeshi na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya wananchi. Kwa utaratibu huo Ufaransa ikaweza kuendeleza ukoloni wake nchini Morocco.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita yaani mnamo tarehe 18 mwezi Februari mwaka 1965 Miladia, Gambia ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muingereza na siku kama hii imepewa jina la siku ya kitaifa nchini humo. Uingereza ilianza kuikoloni Gambia mwaka 1588 Miladia na kupora maliasi za nchi hiyo kwa karibu karne nne. Mwaka 1963, Uingereza iliipatia Gambia uhuru usio kamili kufuatia kudhoofika kisiasa na kiuchumi katika Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa kuendeleza ukoloni wake. Na hatimaye ilipofika mwaka 1965 Gambia ikajipatia uhuru wake kamili. Gambia ni nchi ya kwanza kuwahi kukoloniwa na Uingereza barani Afrika.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, wananchi Waislamu wa Tabriz huko kaskazini magharibi mwa Iran walikutana katika moja ya misikiti mikubwa ya mji huo kwa lengo la kuwakumbuka wananchi waliouawa shahidi tarehe 19 mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya huko Qum kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani. Wenyeji wa Tabriz walikutana hapo kufuatia wito uliotolewa na maulamaa na wanazuoni wa kidini.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita Ayatullah Sayyid Mohammad Swadiq al-Sadr mmoja wa maulamaa mashuhuri wa Iraq aliuawa shahidi na magaidi katika mji mtakatifu wa Najaf nchini humo. Wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maandamano kadhaa kufuatia kuuawa kwa ulamaa huyo mkubwa na kuutaja utawala wa zamani wa Baath huko Iraq kuwa ndio uliomuuwa shahidi Ayatullah Sadr. Utawala wa zamani wa Baahi wa Iraq ulifanya mauaji mengi dhidi ya maulamaa wa kidini katika siasa zake za kuidhoofisha Hauza ya Najaf na wanazuoni wa nchi hiyo, tangu uliposhika hatamu za uongozi huko Iraq mwaka 1968.