Feb 18, 2018 16:26 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 27 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia taarifa ya Baraza la Mji wa New York nchini Marekani ya kuheshimu hisia na imani ya kila mtu wakiwemo Waislamu licha ya kuwekwa marufuku ya kuwazuia raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu kuingia nchi hiyo. Ndugu wasikilizaji mnafahamu kwamba, katika kila shambulizi la kigaidi linalotokea Ulaya na Marekani Rais Donald Trump huwa analihusisha kitendo hicho na Waislamu ambao aghlabu huwa hawana mahusiano yoyote na vitendo hivyo. Lakini katika shambulizi la kigaidi la mjini Las Vegas na kwa kuzingatia ukubwa wake, Trump alifumba mdomo na kushindwa kulitaja kuwa ni shambulizi la kigaidi.

Donald Trump, Rais wa Marekani mwenye chuki ya hali ya juu dhidi ya Waislamu duniani, lakini rafiki mkubwa wa Saudia

Hii ni kwa kuwa muhusika wa shambulizi hilo alikuwa Mmarekani ambaye hakuwa na mfungamano wowote na makundi ya kigaidi, kama ambavyo pia hakuwa na jina la Kiislamu. Pamoja na hayo rais huyo wa Marekani, ameendelea kuwa na mtazamo hasi na wa kibaguzi dhidi ya Uislamu kwa kudai kwamba Waislamu ni tishio dhidi ya usalama wa ndani na nje ya Marekani. Kati ya hatua za kibaguzi dhidi ya Uislamu zilizotekelezwa hivi karibuni na rais huyo wa Marekani ni kuutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Kizayuni pamoja na kutuma jumbe tatu tata katika mtandao wa kijamii wa Twitter za chuki na kibaguzi katika kumpongeza kiongozi wa kundi linaloeneza chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza. Kuenea kwa jumbe hizo kulikabiliwa na radiamali kali za walimwengu na hata barani Ulaya hususan nchini Uingereza kwenyewe. Katika uwanja huo, Theresa Mary May, Waziri Mkuu wa Uingereza aliikosoa vikali hatua ya Trump ya kutuma jumbe hizo ambazo pia zilikuwa zinamuunga mkono Jayda Fransen, kiongozi wa kundi la mrengo wa kulia linaloendesha kampeni za chuki za Britain First nchini humo.

Jayda Fransen kulia, kiongozi wa kundi la mrengo wa kulia linaloendesha chuki dhidi ya Uislamu Uingereza

Mtazamo wa walio wengi nchini Uingereza na hasa viongozi wa nchi hiyo, waliichukulia hatua ya Trump ya kuunga mkono video za chuki dhidi ya Uislamu za Jayda Fransen, kuwa si tu kwamba ilichochea harakati ya chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu, bali pia ililenga kuchafua usalama na amani ya kijamii nchini Uingereza sambamba na kusaidia kupanua mirengo na makundi yenye kufurutu ada na ukatili ndani ya taifa hilo. Katika uwanja huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ililitaja kundi la Britain First kuwa kundi linaloeneza siasa za chuki na ukatili ndani ya nchi hiyo. Hata hivyo baada ya radiamali hizo juu ya ujumbe wa Twitter wa rais huyo wa Marekani, Trump kwa mara nyingine tena alituma ujumbe mwingine na mara hii akimshambulia Theresa Mary May, Waziri Mkuu wa Uingereza ambapo alisema: "Usiwaze sana juu yangu, badala yake waza juu ya ugaidi wa Uislamu ndani ya Uingereza. Sisi tunajua tunalofanya." Mwisho wa kunukuu.

***************

Ndugu wasikilizaji, wimbi la upinzani la Populism dhidi ya wahajiri hususan Waislamu, limeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni ndani ya nchi za Magharibi. Ni wimbi ambalo kwa mtazamo wa weledi wengi, limeshika kasi baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani.

Jamii ya Waislamu nchini Marekani

Aidha wimbi la Populism limeyafanya hata baadhi ya makanisa barani Ulaya kutengeneza video zinazoeneza propaganda za uongo kwa kudai kuwa eti Waislamu na wahajiri ni magaidi na hivyo kupandikiza mbegu ya chuki na ubaguzi kwa makundi ya mrengo wa kulia barani humo kuwalenga wafuasi wa dini hiyo ya mbinguni. Video zilizomfanya Trump kumuunga mkono Jayda Fransen, kiongozi wa kundi la kigaidi la Britain First, ni kati ya video hizo za uongo. Mwanzoni mwa moja ya video hizo anaonyeshwa Muhajiri mmoja Mwislamu akimshambulia kijana mdogo wa Uholanzi, suala ambalo hata hivyo lilikadhibishwa na viongozi wa Uholanzi kwenyewe ambao walisema kuwa, mtu ambaye ameonyeshwa katika video hiyo hakuwa muhajiri, bali ni mtu aliyezaliwa nchini Uholanzi. Ama video ya pili, inamuonyesha mtu mmoja akivunja sanamu la Bi Maryam (Bikira Maria), ambapo hata hivyo haikufahamika video hiyo ilichukuliwa sehemu gani na nchi gani. Baadhi ya vyombo vya habari vilidai kwamba, inaonekana video hiyo ilichukuliwa nchini Syria ikiyahusisha makundi ya kigaidi na ya Kiwahabi.

Genge la Daesh (ISIS) linalochafua sura ya Uislamu kupitia mkakati wa madola ya Magharibi

Na video ya tatu iko wazi na inahusiana na ghasia za wananchi wa Misri mwaka 2013 ambapo inamuonyesha mtu mmoja akiangushwa na watu wengine kutoka juu ya nyumba. Watu hao walihukumiwa jela mwaka 2015 nchini Misri huku mmoja wao akihukumiwa kunyongwa kwa kitendo hicho. Ukweli ni kwamba, Trump anafanya mambo ambayo yanamvua sifa ya kuwa rais wa nchi kiasi kwamba bila kufahamu au kwa makusudi anayaunga mkono makundi ya kigaidi yanayoendesha chuki dhidi ya Uislamu kwa madai ya kudhamini usalama wa Marekani tena nje ya mipaka ya nchi yake. Suala ambalo hata hivyo limepelekea kuwepo mpasuko mkubwa kati ya Marekani na washirika wake tokea aingile madarakani ikulu ya White House. Kwa hakika suala hilo linaweka wazi miamala na siasa hasi za Marekani dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla kote duniani.

**************

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Ama kuhusiana na suala la kuutambua mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel si tu kwamba hakuna muitifaki yeyote wa Marekani ambaye amekubaliana nalo, bali wamelitaja kuwa linaloweza kuibua ghasia na machafuko sambamba na kuvuruga anga ya mazungumzo yanayoytajwa kuwa ya amai kati ya utawala huo na Wapalestina.

Abdel Bari Atwan, mwandishi mashuhuri wa gazeti wa Kiarabu na mhariri mkuu wa gazeti la Rai al-Youm

Kwa hakika hatua hiyo ya Trump iliakisiwa sana kwa sura hasi kati ya nchi za Magharibi na hata katika fikra za Waislamu walio wengi. Abdel Bari Atwan, mwandishi mashuhuri wa gazeti wa Kiarabu na mhariri mkuu wa gazeti la Rai al-Youm akituma ujumbe kuhusiana na hatua ya Trump kuutambua mji huo kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni alisema: "Trump ni rais mbaguzi sana, mlaghai na mtu mwenye chuki ya hali ya juu dhidi ya Uislamu na Warabu. Ukweli ni kwamba, Trump ni mtu wa karibu sana wa Benjamin Netanyahu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Trump anasikiliza tu maneneo ya Jared Corey Kushner, mume wa binti yake (Ivanka Trump). Ushirikiano huo wa muda mrefu ambao ulichangia katika mradi wa ujenzi wa vitongozi vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo ni mali ya Waislamu na Waarabu, hii leo pia unaendelea kushuhudiwa moja kwa moja kutoka kwa rais huyo wa Marekani." Mwisho wa kunukuu.

Masjidul-Aqsa ambayo inakabiliwa na hatari kubwa ya Mzayuni

Kadhalika Abdel Bari Atwan aliongeza kwa kusema: "Ninatoa ujumbe kwa taifa la Palestina kusimama imara kupinga mwenendelezo wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi, dhidi ya Trump, dhidi ya Netanyahu na dhidi ya viongozi wala njama wa Kiarabu ambao wanashirikiana moja kwa moja na Trump na Israel. Wale ambao katika Intifadha ya kwanza walisimama kwa mawe, wale waliosimama katika Intifadha ya pili kwa silaha na wale waliosimama katika Intifadha ya tatu kwa kisu, wote wanatakiwa kusimama imara kukabiliana na njama hizo chafu." Mwisho wa kunukuu.

******************

Baada ya hayo sasa tuelekeze dira ya kipindi hiki katika ushindi wa jeshi la Iraq dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchini humo. Ndugu wasikilizaji baada ya jeshi la Iraq kutangaza kukamilisha operesheni za kulisafisha eneo la kijani la mji wa Baghdad hapo tarehe tisa Disemba mwaka jana, wakazi wa mji huo walishuhudia kupaa angani helikopta na ndege za kijeshi kama ishara ya kumalizika operesheni hizo dhidi ya genge la kigaidi la Daesh. Kufuatia mafanikio hayo Waziri Mkuu Haider Jawad Kadhim al-Abadi na ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa jeshi la Iraq aliitangaza tarehe 10 Disemba kuwa siku ya likizo. Kadhalika yalifanyika maonyesho ya kukabiliana na propaganda na fikra za Daesh siku ya Jumatano ya tarehe 13 ya mwezi huo wa Disemba. Maonyesho hayo yalihudhuriwa na zaidi ya wataalamu 120 kutoka nchi 42 za dunia.

Trump na njama zake za kutaka kuipora Masjidul-Aqsa

Aidha katika maonyesho hayo ambayo yalisimamiwa na Haider al-Abadi mwenyewe, kulionyeshwa vifaa vya kukabiliana na fikra za Kiwahabi za Daesh. Kadhalika kuwekwa wazi tajriba yenye thamani kubwa ya taifa la Iraq katika mapambano yake ya kuwashinda magaidi na kadhalika kusaidia kudhamini usalama na amani ya dunia, ni miongoni mwa maudhui zilizowasilishwa katika maonyesho hayo.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 27 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

Tags