Feb 24, 2018 00:46 UTC
  • Jumamosi, 24 Februari, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1439 Hijria mwafaka na tarehe 24 Februari 2018 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 914 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhaat Hamedani mwenye lakabu ya Abul Fadhl, aliuawa shahidi kwa kunyongwa mjini Hamedan Iran. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi na malenga mahiri. Ainul Qudhaat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo katu hakuwa akiogopa kubainisha itikadi zake. Ni kutokana na misimamo yake hiyo thabiti ambapo mwaka 525 Hijria alitiwa mbaroni na kufungwa huko Baghdad. Baada ya muda alihamishiwa Hamedan nchini Iran na kunyongwa kando na shule yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Tamhiidat na Haqaiqul Qur’an. ***

Ainul Qudhaat Hamedani

 

Miaka 796 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia huko Cairo Misri, Bahauddin Abul Abbas maarufu kwa jina la Qadh ashraf, alimu na msomi wa Kimisri. Kama alivyokuwa baba yake, Bahauddin pia alikuwa kadhi mahiri na alijishughulisha na kazi hiyo mjini Cairo. Alisifika kwa akili na upeo mkubwa na katika maandiko yake alikuwa akifuata mtindo wa uandishi wa baba yake. ***

Qadh ashraf

 

Katika siku kama ya leo miaka 493 iliyopita, alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno. Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri na shujaa. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads." Mshairi huyo mahiri wa Kireno aliaga dunia mwaka 1580. ***

Luis Vaz de Camoens

 

Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita, utawala wa muda au duru ya pili ya mfumo wa jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kuendesha mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme dikteta wa nchi hiyo. Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 69 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes kilichoko katika bahari ya Aegean. Ni vyema kutaja hapa kuwa, baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu.***

Mkataba wa kusitisha mapigano kati ya Misri na Israel

 

 

 

Tags