Apr 17, 2018 10:32 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (34)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 34.

Kwa wale wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika sehemu iliyopita ya 33 tulieleza kwamba Sheikh Yusuf Al-Qardhawi ni mmoja wa watu ambao wamekuwa na nafasi kubwa katika ubunifu wa nadharia ya harakati potofu ya Utakfiri, kwa maana ya ukufurishaji na kufarakanisha umma katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tukaeleza kwamba, kwa hatua yake ya kuitilia shaka fatua ya kihistoria ya Sheikh Mahmoud Shalt’ut ya kujuzisha Waislamu wa madhehebu za Suni kufuata hukumu za kiibada za madhehebu ya Jaafari, ambayo ni maarufu kama Shia'tul-Imamiyyah Al-Ithnaashariyyah, Qardhawi amekuwa sababu ya kufufuka tena mielekeo ya hisia za chuki na uadui dhidi ya Shia katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kufanya hivyo Qardhawi alisema yeye, kwa kushirikiana na Sheikh Ahmad Al-Asal, mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Islamabad, Pakistan walifanya kazi ya kukusanya na kutayarisha vitabu vinne vilivyoandikwa na Sheikh Shalt’ut, lakini hajawahi kuona katika maandiko yake kama amesema kitu kama hicho. Lakini tukatoa ushahidi wa makala ya jarida la Al-Bashaair ambalo katika toleo lake la tarehe 14 Machi mwaka 2009 liliandika makala na kumnukuu Sheikh Jamal Qut’b, mmoja wa maulamaa wa Al Azhar akieleza kwamba Qardhawi na Al-Asal hawakukusanya maandiko yote ya Sheikh Shalt’ut. Aidha tukanukuu makala iliyoandikwa na Sheikh Isam Talima kwa anuani isemayo: “Naam, Sheikh Shalt’ut ametoa fatua ya kujuzisha kufuata madhehebu ya Jaafari katika masuala ya kiibada.”

Katika makala yake hiyo, Sheikh Isam anaendelea kueleza kwamba, ni wazi kuwa Sheikh Shaltut alikuwa na imani kamili juu ya fatua yake aliyotoa. Hilo halikuwa suala kwamba yeye ametoa fatua tu, na kwa kufanya hivyo ameshamaliza kazi yake. Lakini muda mfupi baada ya kutoa fatua hiyo jarida la Al-Mujtamau'l-Arabi lilifanya naye mahojiano marefu ambayo yalikuja kuchapishwa tena yote kamili na gazeti la Al-Ahram. Hata hivyo Sheikh Talima anamalizia makala yake kwa kusema kuwa licha ya hima na bidii kubwa iliyofanywa na Al-Azhar si athari zote za Sheikh Mahmoud Shalt’ut zilizoweza kukusanywa, na ikiwa Qardhawi na Asal hawakuwahi kuiona fatua hiyo, sababu yake ni kwamba Asal alielekea Qatar mwaka 1960, naye Qardhawi alihama Misri na kuelekea huko mwaka 1961wakati Sheikh Shaltut aliaga dunia mwaka 1963. Katika kipindi hicho makala na maandiko mbalimbali muhimu ya Shalt’ut ambayo yalikuwa hayajakusanywa rasmi yalichapishwa; na hivyo vitabu ambavyo Qardhawi na Asal walivikusanya vinahusiana na kipindi cha kabla ya kutolewa fatua ya Shalt’ut, na ni wazi kwamba hadi wakati huo Sheikh Shalt’ut alikuwa bado hajatoa fatua hiyo hata iwe katika maandiko yaliyokusanywa na wawili hao.

 

Kueneza chuki dhidi ya Ushia ni moja ya misingi mikuu ya tapo na harakati ya ukufurishaji; na mtazamo huo unawasha na kukoleza moto wa mfarakano, vita na umwagaji damu baina ya Waislamu. Miongoni mwa visingizio vinavyotumiwa na harakati hiyo potofu kuhalalisha na kutilia nguvu madai yao ya kuwakataa Mashia kama Waislamu ni tuhuma zao za uongo kwamba “Shia wana itikadi ya kuamini kwamba Qur’ani imepotoshwa”. Wakati wafuasi wa madhehebu moja wanapotuhumiwa kwamba hawaiamini Qur’ani iliyopo huwa ni rahisi kueneza na kuwanasibishia itikadi nyengine potofu na kuwatuhumu kuwa wana itikadi zisizo za kitauhidi. Na hii ni katika hali ambayo maulamaa mbalimbali wakubwa wa Kishia kuanzia wa zamani kama marehemu Sheikh Saduq (RA) mpaka wa zama hizi kama marehemu Imam Khomeini (RA) pamoja na wanafunzi wake kama marehemu Ayatullah Ma'refat (RA) wote kwa pamoja wamesisitiza kwa uwazi kabisa kwamba Qur’ani iliyopo ni sahihi wala haina chochote kilichopotoshwa ndani yake.

Kuzichukulia itikadi za Kishia kuwa zina chimbuko la Uyahudi, ni tuhuma nyengine chafu ambazo zinatolewa mara kwa mara na Masalafi. Kwa kawaida maudhui hii huzungumziwa kwa kufungamanishwa na kisa cha Abdullah Ibn Saba’a. Kwa mujibu wa kisa hicho cha kutunga myahudi mmoja katika watu wa Yemen ambaye kidhahiri alijifanya kuwa amesilimu, ndiye aliyeanzisha fikra na itikadi za Kishia kulingana na mafundisho ya Kiyahudi na yeye pia ndiye mwasisi wa itikadi za Ushia. Baadhi ya Masalafi kama Saadi Mahdi Al Hashemi, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ummul-Qura nchini Saudi Arabia ametumia kisa hicho na kuwanasibisha wapokezi wa Hadithi wa Kishia pia na Uyahudi. Kuhusiana na tuhuma hizo, Allamah Askari (RA) amethibitisha katika utafiti na uhakiki aliofanya kuwa shakhsia ya mtu aitwaye Abdullah Ibn Saba’a ni bandia na ya kubuni. Tuhuma na madai mengine yaliyosalia yanayotolewa kuhusu Ushia huwa chimbuko lake ni masuala mawili hayo ya msingi au maudhui nyengine za ziada.

 

Bila shaka harakati za kuzusha mifarakano katika safu za Waislamu haihusiani na Masuni tu kupitia matapo ya Kisalafi na Kitakfiri. Miongoni mwa Mashia pia kuna watu na makundi yanayochochea na kukoleza moto wa hitilafu na uadui baina ya Waislamu kwa kuwavunjia heshima viongozi wakubwa wa dini ya Uislamu na masahaba wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa mfano, katika hatua chafu na ambayo haihalalishiki wala haiwezi kutetewa, mtu mmoja aliyevalia vazi la alimu wa dini wa Kishia aliwahi kusimama mbele ya chombo cha habari na kutoa maneno ya kashfa na ya kumvunjia heshima mke wa bwana Mtume SAW bibi Aisha ambaye anaheshimika mbele ya Ahlu-Sunnah. Maneno ya mtu huyo yaliwachochea Waislamu wa Kisuni dhidi ya wenzao wa Kishia hususan katika nchi za Kiarabu. Nchi ya Kuwait ilimpokonya uraia mtu huyo. Katika upande mwengine, watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka wakatangaza zawadi maalumu ambayo watampa atakayemuua mfitini huyo. Hata hivyo watu wengi wanaitakidi kwamba mtu huyo aliyekuwa amevalia vazi la kidini la shekhe wa Kishia na anayewasha moto wa fitna ya kuleta mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu, hakuwa shekhe wala alimu wa dini asilani; na kwa miaka kadhaa tangu alipotoroka Kuwait na kupewa hifadhi ya ukimbizi nchini Uingereza pasi na kusoma kwenye chuo cha kidini cha Kishia ameamua kuvaa vazi la alimu wa dini na kupanda kwenye minbari hii na ile kufanya kazi ya kutusi na kuchochea mfarakano baina ya jamii za Kiislamu. Ni jambo lililo wazi kwamba katika zama hizi ambapo ulimwengu mzima wa kikoloni umepanga safu kukabiliana na Uislamu, lengo lake likiwa ni kuufuta Uislamu, hatua hii na harakati nyenginezo za kimatapo na kimadhehebu zenye lengo la kuzitumbukiza kwenye mizozo na machafuko jamii za Kiislamu, bila shaka ni fimbo na silaha ya kikoloni; na kwa sababu hiyo Ushia wa Kiingereza ni jina mwafaka inalostahiki kupewa harakati hiyo.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 34 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Tags